Mlima Nyiragongo: Volcano iliyolipuka yasababisha watu kukimbia makazi yao DRC

Lava ikimwagika kutoka kwenye mlima Nyiragongo

Chanzo cha picha, Reuters

Maelfu ya watu wamekimbia makazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya volkano kubwa kulipuka.

Chemchemi za lava kubwa zilitoka kwenye Mlima Nyiragongo kwa kulipuka angani usiku na kutengeneza wingu zito jekundu juu ya mji wa Goma, ambao una wakazi milioni mbili.

Mtiririko wa lava ulifika uwanja wa ndege wa jiji lakini imeripotiwa sasa umesimama.

Volkano hiyo, iliyoko 10km (maili sita) kutoka Goma, ililipuka mara ya mwisho mnamo 2002 na kuua watu 250 na kuwafanya watu wengine 120,000 kukosa makazi.

Wakati wa asubuhi ya Jumapili, wakaazi wengi walivuka mpaka wa karibu wa Rwanda, wakati wengine walikwenda kwenye viwanja vya juu magharibi mwa jiji.

Umati ulionekana na magodoro na mali nyingine, wakikimbia hata kabla ya tangazo la serikali, ambalo lilikuja saa kadhaa baada ya mlipuko kuanza.

Mamlaka ya Rwanda ilisema karibu watu 3,000 walikuwa wamevuka kutoka Goma. Vyombo vya habari vya serikali nchini humo vilisema watalazwa katika shule na sehemu za ibada.

Mkazi mmoja wa Goma, Richard Bahati, alisema alikuwa nyumbani kwake aliposikia mayowe. "Nilitoka nje na kuona anga lilikuwa jekundu. Nina wasiwasi sana, nina wasiwasi sana. Niliishi kupitia shida na volkano hii mnamo 2002. Volkano iliharibu nyumba zetu zote na mali. Ndio maana ninaogopa tena wakati huu."

"Kila mtu anaogopa, watu wanakimbia. Kwa kweli hatujui la kufanya," mkazi wa eneo hilo Zacharie Paluku aliliambia shirika la habari la Associated Press.

Chanzo cha picha, EPA

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Getty Images

Umeme ulikuwa ilikatika katika maeneo makubwa, na barabara kuu inayounganisha Goma na jiji la Beni ilifunikwa na lava. Kulikuwa pia na ripoti za matetemeko ya ardhi.

"Kuna harufu ya Sulphur. Kwa mbali unaweza kuona miale mikubwa ikitoka mlimani," mkazi Carine Mbala aliliambia shirika la habari la AFP.

Afisa kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga, ambako volkano iko, alisema katika barua kwa wafanyakazi kwamba mlipuko huo ulikuwa sawa na ule wa 2002 na kwamba kila mtu karibu na uwanja wa ndege anapaswa "kuhama bila kuchelewa".

Watu wameshauriwa kutulia, lakini wengine walilalamika juu ya ukosefu wa habari kutoka kwa mamlaka.

Waziri wa Mawasiliano Patrick Muyay alisema kwenye mtandao wa Twitter kwamba serikali ilikuwa ikijadili "hatua za haraka" baada ya waziri mkuu kuitisha mkutano wa dharura katika mji mkuu, Kinshasa.

Lakini baadaye, Bwana Muyay alisema nguvu ya mtiririko wa lava imepungua na tathmini ya hali ya kibinadamu inaendelea.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini, Monusco, ulisema ulikuwa ukifanya upelelezi kwa ndege juu ya jiji hilo.

Mlima Nyiragongo ni moja ya milima hai zaidi ulimwenguni lakini kulikuwa na wasiwasi kwamba shughuli zake hazikuzingatiwa vizuri na Kituo cha Volcano cha Goma, tangu Benki ya Dunia ilipokata fedha kwa sababu ya madai ya ufisadi.

Katika ripoti ya Mei 10, uchunguzi ulionya kuwa shughuli za matetemeko ya ardhi huko Nyiragongo zimeongezeka.

Mwaka jana, mkurugenzi wa uchunguzi huo, Katcho Karume, aliiambia BBC kwamba ziwa la lava la volkano lilikuwa limejaa haraka, na kuongeza nafasi ya mlipuko katika miaka michache ijayo. Lakini pia alionya kuwa tetemeko la ardhi linaweza kusababisha janga mapema.

Mlipuko mbaya zaidi wa volkano ulitokea mnamo 1977, wakati zaidi ya watu 600 walifariki.

Map