Mzozo wa Israel na Palestina : Wapatanishi wanavyotafuta kuimarisha suluhu

Uharibifu mji wa Beit Hanoun, ukanda wa Gaza

Chanzo cha picha, EPA

Wakati Gaza na Israeli zinaibuka kutoka kwenye siku 11 za mizozo, wapatanishi wanatafuta kuimarisha suluhu hiyo na kuzuia vurugu zaidi kwa muda mrefu.

Timu ya Wamisri ilikuwa Israeli Jumamosi, wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akitarajiwa kuzuru eneo hilo wiki ijayo.

Israeli na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas wamedai ushindi katika mzozo wa hivi karibuni.

Zaidi ya watu 250 waliuawa, wengi wao mjini Gaza.

Mapigano yalianza Mei 10 baada ya wiki kadhaa za mvutano ulioibuka ambao ulimalizika kwa mapigano huko al-Aqsa, eneo takatifu linaloheshimiwa na Waislamu na Wayahudi,eneo linalokaliwa la Yerusalemu Mashariki. Hamas ilianza kufyatua roketi baada ya kuionya Israeli ijiondoe kwenye eneo hilo,hali iliyosababisha visasi.

Tangu makubaliano hayo yaanze kutekelezwa Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema kudhalilishwa kwa nguvu ya jeshi la Hamas kwa kulipuliwa kwa bomu angani ilikuwa "mafanikio ya kipekee".

Aliongeza: "Ikiwa Hamas inadhani tutavumilia mvua ya roketi, ni makosa" na kuahidi "kiwango kipya cha nguvu" kujibu.

Wakati huo huo, Hamas imezungumza juu ya kile ilichokiita "furaha ya ushindi" na kiongozi wake Ismail Haniyeh alisema kuwa mzozo huo "umefungua mlango wa awamu mpya ambazo zitashuhudia ushindi mwingi".

Chanzo cha picha, EPA

'Maisha yatarejea'

Mkataba ulitekelezwa siku yake ya pili Jumamosi. Masharti yake hayajulikani. Israeli ilisema tu kwamba imekubali kusitisha uhasama "kwa pande zote na bila masharti".

Misri, Qatar, Marekani na Umoja wa Mataifa zinaonekana kuhusika.

Siku ya Jumamosi, Baraza la Usalama la umoja wa mataifa lilitoa taarifa yake ya kwanza kuhusu mzozo huo, ikiwasifu wapatanishi na kutaka "kuzingatiwa kikamilifu kusitisha mapigano".

Timu za wapatanishi wa Misri zimekuwa zikiingia kati ya Gaza, Israel na Ukingo wa Magharibi.

Mwanadiplomasia wa Misri alisema timu hizo zinatekeleza hatua zilizokubaliwa na kujaribu kuzuia mazoea ambayo yalisababisha mapigano ya hivi karibuni, lakini hakukuwa na taarifa za kina.

Bwana Blinken anatarajiwa kutembelea eneo hilo juma lijalo. Mpango huo haujatolewa lakini chanzo cha Marekani kilisema atasafiri kwenda Israeli na Ukingo wa Magharibi Jumatano na Alhamisi. Anaweza kutembelea Misri na Yordani. Marekani haitafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas, ambayo inaiona kama shirika la kigaidi.

Tom Bateman wa BBC, ambaye amekuwa huko Gaza, anasema kuwa, ingawa utulivu umekaribishwa hapo, watu wengi wanajua labda inamaanisha tu kuhesabu mzozo unaofuata ambao hauepukiki.

Raia wa pande zote mbili wamesema kuhusu kutaka kuishi bila hofu ya kushambuliwa kutoka angani.

Lakini wengi hawajiamini. Mmiliki mmoja wa duka huko Gaza, Ashraf Abu Mohammad, aliliambia shirika la habari la Associated Press: "Maisha yatarudi, kwa sababu hii sio vita ya kwanza, na haitakuwa vita ya mwisho."

Ghazi Dahdouh hawezi kwenda nyumbani tena kwa sababu nyumba yake ililipuliwa na kombora lililorushwa kutoka kwenye ndege ya kivita ya Israeli. Kwa hivyo anaishi juu yake. lakini ukitembea juu kifusi na katikati ya paa la saruji iliyoanguka utampata Ghazi, 70, kwenye hema.

Anasema atakaa mpaka nyumba yake ijengwe tena. Chini ya turubai Ghazi ananiambia mtoto wake ni polisi alilipwa nusu ya mshahara. Ghazi akampa yeye na wajukuu wake vyumba viwili ndani ya nyumba.

Israeli ilisema wakati wa mzozo huo ilizipiga nyumba za wanamgambo, ikisema kuwa walikuwa na malengo halali ya kuzuia mashambulio.

"Mimi ni raia asiye na hatia, sina uhusiano wowote na siasa," Ghazi ananiambia. "Ikiwa nina silaha sasa nitakwenda kupigana, kwa sababu sina hatia. Sina uhusiano wowote na kile kilichonipata."

Ghazi hawezi kuelewa ni kwanini yeye na familia yake ya karibu wanapaswa kuachwa bila makazi. Anasema: "Ikiwa wanamtafuta [mwanangu] kwa sababu yeye ni polisi wangepaswa kuniambia nisimruhusu aishi hapa, badala ya kubomoa jengo lote."

Vikundi vya haki hapo awali vilishutumu Israeli kwa kushindwa kutoa ushahidi wazi kwamba kuharibu nyumba kwa njia hii ni sawa na lengo halali la jeshi chini ya sheria za kimataifa.

Msafara wa kwanza wa misaada ya kibinadamu umewasili Gaza. Malori zaidi yalifika katika kivuko cha Israeli cha Kerem Shalom Jumamosi na msafara wa magari 130 ulipangwa kuvuka kutoka Misri.

Lakini Shirika la Afya Ulimwenguni limesema vituo vya afya vya Gaza viko katika hatari ya kuzidiwa na maelfu ya watu waliojeruhiwa.

Lynn Hastings, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa UN kwa maeneo ya Wapalestina, alisema kutoka Jiji la Gaza alikuwa na matumaini kuwa utulivu utabaki.

Lakini alikuwa amezungumza na familia na "wanahisi kuwa hawana udhibiti wa maisha yao".

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa takriban miaka 14, Gaza imekuwa chini ya kizuizi kwenye mipaka yake na Israeli na Misri ambayo inazuia kupitisha watu na bidhaa - moja ya suala kuu kwa upatanishi wowote wa siku zijazo.

Israeli inasema lazima ipunguze upatikanaji wa silaha wa Hamas, kwani wanamgambo wanakataa kushusha silaha. UN inasema zuio lazima kimalizike kwa uchumi wa Gaza kuimarika.