Aliko Dangote: Kutoka kuikosoa Tanzania kimataifa mpaka kuahidi uwekezaji zaidi na kuitangaza

Dangote na Rais Samia

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Mwezi Oktoba mwaka 2017, akiwa katika mkutano mkubwa wa wakezaji jijini London, bilionea wa Nigeria Aliko Dangote alikosoa vikali sera za uwekezaji nchini Tanzania.

Maneno aliyoyasema Dangote wakati huo na aliyoyasema jana akiwa Ikulu jijini Dar Es Salaam ni tofauti kabisa, na yawezekana yakaendeleza mjadala wa utofauti baina ya rais wa sasa wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hasssan na mtangulizi wake hayati John Pombe Magufuli.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na jarida maarufu la habari za biashara, The Financial Times, Dangote ambaye wakati huo alikuwa tayari ameshafanya uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha saruji Tanzania alisema sera za uwekezaji nchini humo zinawaogopesha wawekezaji kutoka nje.

Dangote pia alimuonya aliyekuwa rais wa Tanzania wakati huo hayati John Magufuli kuwa wakati umefika "kuzipitia upya sera zake ama akubali kuingia katika hatari ya kuwapoteza wawekezaji wote nchini humo."

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Maelezo ya picha,

Miaka minne baada ya kukosoa vikali sera za uwekezaji Tanzania, Dangote asema atashawishi wawekezaji kurejea nchini humo.

"...sheria mpya zinazoundwa Tanzania zinaiweka nchi hiyo kwenye hatari ya kuwafukuza wawekezaji wote na kushindwa kuwarejesha tena," alisema Dangote.

Wakati akiyasema hayo, hayati Magaufuli alikuwa yupo katika kile alichokiita vita ya kiuchumi ambapo awali mwaka huo alianzisha uchunguzi wa kina katika sekta ya madini na 'kubaini uhalifu mkubwa' ambao ulisababishwa kuundwa kwa sheria mpya ya madini.

Mwisho wa mzozo huo wa madini ukazaa maafikiano na kampuni kubwa ya madini ulimwenguni ya Barrick na kuunda kwa pamoja na serikali kampuni mpya ya kuchimba madini ya Twiga.

'Milango imefunguka'

Mara baada ya kuingia madarakani mwezi Machi mwaka huu kufuatia kifo cha Magufuli, Rais Samia hakumung'unya maneno kuhusu hali ya uwekezaji nchini humo.

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Maelezo ya picha,

Dangote akutana na Rais Samia na kusema mambo yamebadilika Tanzania

Katika hotuba zake za mwanzo, alikemea ubabe wanaofanyiwa wawekezaji pamoja na kutotabirika kwa sera za uwekezaji pamoja na kodi.

Rais Samia pia alizungumzia suala la kupewa vichocheo (incentives) kwa wawekezaji wakubwa ili walete miradi nchini Tanzania.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya biashara na uchumi wanaamini kuwa kulikuwa na mvutano baina ya Dangote na serikali ya Magufuli katika utekelezwaji wa vichocheo ambavyo mwekezaji huyo aliahidiwa na aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye ndiye alimkaribisha Tanzania.

Akiwa Ikulu jana, Dangote amesema kuwa: "mazingira ya kibiashara yamebadilika ghafla na milango imefunguka... na sasa popote pale nitakapokwenda nitainadi Tanzania na kuwaambia watu kuwa mambo yamebadilika na kila mmoja arejee na kuwekeza kwa nguvu."

"Nimempongeza (Rais Samia) kwa mabadiliko muhimu anayoyaleta ... Tutaendeea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa wananchi, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania."