Wake wa marais: Mfahamu mke wa rais wa DRC Denise Nyakeru Nkana Tshisekedi

  • Dinah Gahamanyi
  • BBC Swahili
Hadithi ya maisha ya Bi Denise Tshisekedi imekuwa na kusikitisha kwa upande mmoja na upande mwingine ya kutia moyo

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru/Facebook

Maelezo ya picha,

Hadithi ya maisha ya Bi Denise Tshisekedi imekuwa na kusikitisha kwa upande mmoja na upande mwingine ya kutia moyo

Ni watu wenye ushawishi katika uongozi wa kila siku wa nchi zao, hata hivyo si kila siku utasikia juu ya maisha yao na vipawa vyao. Hawa ni wenza wa marais, ambao baadhi yao ni wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega katika safari za kisiasa za wenza wao mpaka kushika hatamu za madaraka. Wiki hii tunakuletea mfululizo wa makala kuhusu wenza wa marais katika eneo la Afrika Mashariki na Maziwa Makuu ambapo leo katika sehemu ya mwisho tunamuangazia mke wa Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa wengi hadithi ya maisha ya Mke wa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC), Denise Nyakeru Nkana Tshisekedi imekuwa ni ya kuhuzunisha, lakini pia imekuwa ni ya kuwatia moyo baadhi.

Maisha yake utotoni

Denise Nyakeru Nkana alizaliwa tarehe 9 Machi, 1967 katika mji wa Bukavu uliopo katika jimbo la Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Anatoka katika kabila la Abashi, kabila ambalo mume wake sasa Felix Tschisekedi , alilitegemea sana kumuwezesha kupata ushindi wa kura katika wa uchaguzi wa mwaka 2018 kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu nchini Congo.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Denise Nyakeru Tshisekedi alikuwa yatima akiwa na umri wa miezi tisa pekee

Hata hivyo hazungumzi lugha ya mama ya Amashi, kutokana na kwamba alihamia Kinshasa akiwa mchanga, baada ya kifo cha wazazi wake na badala yake anazungumza lugha ya Lingala inayozungumzwa mjini Kinshasa.

Baba yake Denise alikuwa mtoto wa Mama Christine M'ntalushika, na baba yake , Étienne Nyakeru, alikuwa afisa utawala wa jimbo la Kivu chini ya utawala wa kikoloni wa Ubelgiji kabla halijagawanywa na kuwa majimbo mawili sasa-Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

Mauti ya wazazi wake

Ilikuwa ni Tarehe 25 Januari 1968 akiwa mtoto mchanga mwenye umri wa miezi 9 pekee, wazazi wake wawili baba na mama yake walikufa katika ajali ya gari. Kana kwamba haitoshi baba yake mdogo Denise, Joseph Mukombe Banywesize, aliyekuwa nao ndani ya gari hilo alipoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea katika mtaa wa viwanda wa Bukavu.

Inaripotiwa kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari lililokuwa likija mkabala na wazazi wa Denis kuwasha taa zenye mwangaza mkubwa ambao uliwafanya wasiweze kuona mbele na ajali hiyo mbaya ikamuacha Bi Denise ambaye alikuwa kitinda mimba wa familia na ndugu zake saba yatima.

Maisha baada ya kifo cha wazazi wake

Baada ya mkasa huo wa ajali, Bi Denise na ndugu zake wote saba: Nyakeru Naweza Spéciose Christine ; Nyakeru Nabami Stéphanie, Nyakeru Mweze Christophe, Nyakeru Njuma Jeannette; Nyakeru Kalunga John ; Nyakeru Ntalushika Joe-Christian; na Nyakeru Ngami Jean-Paul Franck, wote waliasiliwa na mjomba wao - Ngami Mdahwa Sylvestre ambaye alikuwa Padre mkuu wa Kanisa dogo la Katoliki la jeshi la Congo ilipokuwa ikiitwa Zaire -FAZ- hadi alipofariki mwaka 1985 katika ajali ya barabarani kwenye mtaa wa -Avenue Université mjini Kinshasa.

Masomo na Kazi

Baada ya kifo cha wazazi wake Denise Nyakeru Tshisekedi alilelewa vyema chini ya uangalizi wa dada , kaka zake pamoja na mjomba wake Padre Ngami Mdahwa Sylvestre na aliweza kuendelea na masomo yake vyema na kufaulu mitihani ya shule za msingi na sekondari mjini Kinshasa kwa alama za juu.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Bi. Denise Nyakeru Tshisekedi ni ana taaluma ya uuguzi

Baada ya elimu yake ya sekondari aliamua kusomea uuguzi (Nursing). Alipomaliza masomo yake alikwenda nchini Ubelgiji ambako alifanya kazi ya uuguzi katika makazi mbali mbali ya wazee.

Kazi yake ya kuwahudumia wasiojiweza imempatia Bi Denise heshima hadi leo, ambapo wengi wanamuona kama mama mwenye huruma, mkarimu na mwenye maadili mema ambayo ameyajenga hata kabla hajawa Mke wa rais.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Bi Denise na mume wake Felix Tshisekedi wamejaaliwa na watoto watano- wa kiume mmoja na wa kike wanne.

Akiwa nchini Ubelgiji Bi Denise Nyakeru Tshisekedi alikutana na Bw Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo mwanae Etienne Tschisekedi wa Mulumba na Marthe Kasalu Jibikila ambaye baba yake alikuwa mwanasiasa mkongwe wa upinzani enzi ya Rais wa Zaire Mobutu Seseseko.

Wawili hao walichumbiana na baadaye kuamua kuoana miaka 24 iliyopita na wamejaaliwa na watoto watano - wa kiume mmoja na wa kike wanne- majina yao ni Fanny, Anthony, Christina, Sabrina na wa kitinda mimba, Serena.

Denise Nyakeru kama mke wa rais

Bi Denise alipata cheo cha Mke wa rais mara baada ya mume wake Bwana Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo alipoingia mamlakani mwaka 2019, baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliogubikwa na ghasia.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tschisekedi

Tangu awe Mke wa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Bi Denise ambaye kwa sasa anaitwa "Mke wa rais anayeheshimika sana," amekuwa akijihusisha zaidi katika juhudi za kuimarisha maisha ya wanawake na wasichana wa Congo, kupitia Wakfu uliopewa jina lake ''Foundation Denise Nyakeru Tshisekedi (FDNT)."

Wakfu wa FDNT, ulioanzishwa mwezi Mei mwaka 2019, unashugulikia ajenda nne kama njia ya kutekeleza lengo hilo.

Ajenda ya kwanza ni kuimarisha afya ya wanawake kwa msingi wa sera, Elimu kwa wasichana wadogo hususan kwa wale wanaotoka katika familia zisizojiweza, na mapambano dhidi ya aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana nchini humo.

Bi Denise pia ameazimia kuwajengea uwezo wa kifedha na kiuchumi wanawake akisema kuwa mwanamke mwenye afya njema, mwenye elimu, asiyenyanyaswa, anaweza kuchangia pakubwa maendeleo ya taifa lake.

Kupitia Wakfu wa Denise -''Foundation Denise Nyakeru Tshisekedi (FDNT)" amekuwa akiwahamasisha wanawake na wasichana nchini mwake kuweka bidii katika shughuli zao za kila siku ikiwa ni pamoja na masomo ili kuweza kujikwamua si tu ndani ya DRC lakini kimataifa.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Kama muuguzi mwenye taaluma hiyo, Bi Denise( aliyesimama kushoto) amekuwa akiwatembelea akina mama mjini katika hospitali mbali mbali mjini Kinshasa, kuwashauri juu ya mpango wa uzazi

Akiwa muuguzi aliyesomea, suala la afya ya mama na mtoto limeonekana kuwa moja ya vipaumbele vyake muhimu ambapo amekuwa akitembelea hospitali mbali mbali mjini Kinshasa kuzungumza na wanawake juu ya uelewa wa mpango wa uzazi na pia kuwatia moyo wauguzi na kuwapongeza kwa kazi wanayoifanya.

Chini ya wakfu huu ameweza kuwasaidia vijana wa kike na wa kiume waliofaulu vyema kupata udhamini wa masomo ya ndani na nje ya nchi kupitia mpango aliouita Excellentia.

Katika mkasa wa hivi karibuni wa mlipuko wa Volkano katika Mlima Nyiragongo mjini Goma, Bi Denise alikuwa mstari wa mbele kuwatembelea na kuwapatia msaada wa chakula waathiriwa hususan akinamama na watoto waliopoteza kila kitu, licha ya kwamba baadhi bado hawajaridhishwa na kiwango cha msaada uliotolewa na serikali ya mume wake Bw Felix Tshisekedi.

Majukumu ya kimataifa

Licha ya kwamba amekuwa na madaraka ya Mke wa rais kwa chini ya miaka 3, amepewa majukumu katika utatuzi wa matatizo hususan yale yanayoikabili nchi yake.

Chanzo cha picha, Denise Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Bi Denise Tschisekedi ni Balozi wa nia njema wa Mfuko Umoja wa mataifa wa idadi ya watu (UNFPA)

Bi Denise Nyakeru ambaye kwa sasa pia ni Mke wa Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika kufuatia mme wake kushikilia kiti hicho , amekuwa akiwataka wanawake kushirikiana katika kukabiliana na dhuluma za kijamii, wanazokabiliana nazo katika maisha ya kila siku.

Katika ziara ya hivi karibuni aliyoifanya Rwanda alisema:"Kwetu sisi kuendelea kuwathamini wanawake na familia barani Afrika tunahitaji kufanya kazi pamoja. Pamoja kama wanawake tuko imara sana,"

Bi Denise Tschisekedi ni Balozi wa nia njema wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa idadi ya watu (UNFPA) tangu mwezi Mei 2019, kwa ajili ya mapambano dhidi ya unyanyasaji wenye misingi ya jinsia na kuwezeshwa kwa wanawake.

Aidha alipewa jukumu la "Kuongoza juhudi za kuzuia unyanyasaji wa kingono unaohusiana na mizozo " na Ofisi ya Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na mapambano dhidi ya unyanyasaji huo mwezi Disemba 2019.

Katika wadhifa huo amepewa jukumu la kuwasilisha na kuleta sauti ya waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono katika mikutano na taasisi za ngazi ya juu zaidi za kitaifa, kikanda na katika Umoja wa Mataifa.

Hisia mchanganyiko kumuhusu

Kwa baadhi ya raia Congo hususan wakazi wa mji mkuu wa Kinshasa, Bi Denise Nyakeru Tschisekedi ni mwanamke mwenye maadili na huruma hususan kwa wanawake, wasichana na watoto, na mtu mwenye maono ya kupambana na dhuluma na unyanyasaji mbali mbali unaofanywa dhidi ya wanawake wa DRC.

Chanzo cha picha, Denise Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Raia wa Congo wamekuwa na hisia zinazotofautiana kuhusu namna anavyoshughulikia masuala ya maendeleo ya nchi hususan wanawake

Lakini baadhi ya Wacongo wanaoishi katika majimbo mengine muonekano wake ni tofauti. Wanamlaumu kwa kuendesha shughuli zake Kinshasa pekee na kusahau majimbo mengine.

Raia wa majimbo ya Mashariki mwa DRC Kivu Kusini na Kaskazini wanamuhusisha pia na utawala wa mume wake Felix Tschiseketi ambao wanaulaumu kwa kutojali maendeleo yao kama vile upatikanaji wa huduma za afya, elimu na miundo msingi, huku wakidai Bi Denise kuwa amelisahau eneo alikozaliwa.

''Baadhi hapa wanamuona kama msaliti, kutokana na kwamba anatoka katika ukoo mmoja na mwanasiasa wa upinzani Vital Kamerhe, aliyekuwa raisi wa Bunge lakini kwa sasa Rais Tshisekedi amemfunga na yeye ni mke wake'' aliyaambia makala haya mmoja wa wakazi wa Bukavu.

Baadhi wanamlinganisha na Mke wa mtangulizi wake Bi Olive Lembe di Sita, Mkewe Joseph Kabila ambaye wanasema anawajali zaidi masikini wakielezea mkasa wa hivi karibuni ambapo aligawa viwanja na makazi kwa wakazi wa eneo hilo waliopoteza makazi kufuatia mlipuko wa mlima Volkano wa Nyiragongo.

Muonekano, mtindo mavazi

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru tshisekedi

Maelezo ya picha,

Huonesha hisia za huruma hasa anapokutana na watu wenye shida hususan wanawake na watoto

Kando ya siasa Bi Denise Nyakeru ni mwanamke mwenye muonekano wa uchangamfu hasa anapokutana na kutangamana na watu. Lakini pia huonesha hisia za huruma hasa anapokutana na watu wenye shida hususan wanawake na watoto

Unaweza pia kusoma:

Mtindo wa mavazi

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Maelezo ya picha,

Bi Denise Nyakeru, akiwa na mume wake Rais felix tchisekedi walipokuwa wakiwasili katika tukio la kitaifa mjini Kinshas

Mara kwa mara akiwa katika matukio ya kitaifa na umma Bi Denise Nyakeru huonekana akiwa amevaa mavazi ya Kiafrika kama vile vitenge na batiki, na mara nyingine huongezea kitenge kwenye vazi la kawaida ili kumpatia muonekano wa mama wa Kiafrika na hasa wa Kicongo.

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tschisekedi

Chanzo cha picha, Denise Nyakeru Tshisekedi

Chanzo cha picha, Denise Tshisekedi /Facebook

Maelezo ya picha,

Be Denise Nyakeru tschisekedi pichani akihudhuria maombi ya wanawake, mara nyingine huongezea kitenge kwenye vazi la kawaida ili kumpatia muonekano wa mama wa Kiafrika na hasa wa Kicongo

Katika kipindi cha chini ya miaka 3 baada ya kuwa Mke wa Rais wa jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Bi Denise Nyakeru Tshisekedi, ameonesha juhudi za kushirikiana na mume wake katika kuinua maisha ya wanawake, licha ya kwamba baadhi ya Wacongo wanaona kuwa juhudi zake zinaishia mjini Kinshasa pekee ambako hakuna idadi kubwa ya wanawake na wasichana walioathiriwa na mzozo wa vita vya muda mrefu, ikilinganishwa na Mashariki mwa nchi hiyo.

Lakini baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema, ameanza vyema, apewe muda na huenda juhudi zake zikayafikia maeneo mengine ya nchi., licha ya kwamba matatizo yanayowakumba raia wa DRC kutokana na vita vya muda mrefu huenda yakachukua miaka kupatiwa suluhu.