Raj Kundra:Bwenyenye maarufu India akamatwa kwa kutengeneza video za ngono

Kundra

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bw Kundra na mkewe nyota wa filamu za Bollywood Shilpa Shetty mwaka wa 2015

Katika kesi ambayo imegonga vichwa vya habari, mfanyabiashara maarufu sana nchini India amekamatwa kwa madai ya kutengeneza filamu za ngono.

Raj Kundra, raia wa Uingereza na mume wa nyota wa Bollywood Shilpa Shetty, ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa timu ya kriketi katika Ligi Kuu ya India, mashindano yenye utajiri mkubwa ya kriketi ulimwenguni.

Polisi sasa wanadai Raj mwenye umri wa miaka 45 'anashiriki njama kubwa' ya utengenezaji wa video za ngono ambayo ililazimisha wanawake kadhaa kushiriki na baadaye video hizo zikawekwa mtandaoni.

Hata hivyo, Bwana Kundra amekanusha kutekeleza madai hayo.

Wakili wake Abad Ponda amesema "kukamatwa kwa Bw. Kundra ni kinyume cha sheria".

Watu tisa wamekamatwa kufikia sasa kuhusiana na uchunguzi unaoendelea wa sakata hiyo, ambao ulianza mwezi Februari.

Watu hao ni pamoja na muigizaji, mtayarishaji na mtendaji wa kampuni.

Kulingana na polisi, mshtakiwa alitoa ahadi za uwongo na kuwashawishi wanawake ambao walikuwa wamekubali kufanya matangazo ya biashara na video zinazodaiwa kuwa za ngono.

Chanzo cha picha, Getty Images

Video hizo - zinadaiwa kuchukuliwa katika majumba ya kifahari yaliyokodishwa - kisha zikawekwa kwenye programu za simu za mkononi kwa watumiaji wapatao 400,000 ambao walilipa rupia 200 - 400 (karibu $ 2.70 - $ 5.40; £ 1.95- £ 3.90) kwa mwezi.

Na Bwana Kundra, kulingana na polisi, alikuwa mmiliki wa kampuni inayohusika na video hizo za ngono kwenye majukwaa hayo.

Bwana Kundra alikamatwa kutoka kwenye nyumba yao - jumba kubwa katika jiji la Mumbai - mnamo Julai 20.

Anakabiliwa na mashtaka ya udanganyifu, uuzaji wa maudhui machafu na "matangazo ya maudhui machafu na yasiyofaa.

Chini ya sheria ya India, kuchapisha au kusambaza "maudhui machafu" pamoja na video za ngono ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka saba jela.

Kuwahadaa wanawake

Lakini bado tasnia hiyo inaendelea kustawi nchini humo - umaarufu wake kwa sehemu kubwa umekua na mtandaoni.

Wahindi wanaaminika kuwa miongoni mwa watumiaji wakubwa wa video za ngono mtandaoni - na walishika nafasi ya tatu katika orodha ya nchi zilizochapisha maudhui yake kwenye tovuti ya ngono ya Pornhub, ambayo ndio kubwa zaidi na yenye video za ponografia, baada ya Marekani na Uingereza.

Mnamo Februari 4, 2021, kikundi cha maafisa wa polisi wa Mumbai - waliokuwa wamedokezewa kinachoendelea na mtu asiyejulikana - walitembea kupitia milango ya chuma ya jumba hilo la kifahari la ghorofa moja kaskazini mwa jiji, ambapo inasemekana filamu ya ngono ilikuwa inachukuliwa.

Walikuwa Madh, kitongoji kidogo cha kaskazini mwa Mumbai, na eneo maarufu la kutengeneza filamu.

Polisi walisema walipata watu wawili kwenye kochi wakiwa wamekaa uchi kwa namna ya kuendeleza " maudhui machafu".

Pia walimpata mwanamke mwingine aliyekuwa akiwachukua video, walisema.

Simu za mkononi, kompyuta ndogo au vipakatalishi, na kamera na maudhui ya ngono vilipatikana kwenye nyumba hiyo, polisi walisema.

Watu watano, pamoja na mtu anayesaidia kuchukua filamu, walizuiliwa.

Aidha, mwanamke ambaye polisi ilisema alikuwa analazimishwa kukaa mkao fulani ili achukuliwe video aliokolewa.

Huu ulikuwa mwanzo wa uchunguzi wa muda mrefu wakati ambapo wanawake wengine pia kadhaa, ambao walidai kulazimishwa kushiriki kwenye video hizo za ngono waliwasilisha malalamishi yao.

Picha zawekwa katika mitandao ya kijamii

Polisi walisema mwanamke huyo na wengine wangeweka filamu za ponografia kwenye programu ya simu ya mkononi ambayo ilifuata mtindo wa kuonekana kwa waliojisajili.

Filamu hizo pia zilitangazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Aidha, filamu hizo zilipigwa katika maeneo ya vijijini- yaliyokodishwa kwa siku hiyo katika vitongoji vya Mumbai.

"Waigizaji wapya wa kike wanaotamani kuingia kwenye tasnia ya uigizaji walishawishiwa na watuhumiwa, wakiwaahidi kupata uhusika katika filamu fupi fupi na michezo ya kwenye tovuti", alisema kamishna wa polisi anayehusika na uchunguzi wa uhalifu huko Mumbai, Milind Bharambe.

Mbali na programu ya Hits Moto, programu zingine tatu pia zinachunguzwa.

Bwana Bharambe amesema, polisi wamesitisha rupia milioni 75 [karibu $ 1m; Pauni 730,000] katika akaunti za benki za programu zingine huku uchunguzi kuhusu uhalifu huo ukiendelea

Polisi wanasema kuna mambo makuu mawili kwa kesi hiyo: kuwakamata wale ambao wanatengeneza filamu hizo za ngono, na wale wanaozitangaza.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wachunguzi wanasema pia wanachunguza Kampuni yenye makao yake nchini Uingereza iitwayo Kenrin - wanadai kwamba Bwana Kundra aliuza programu ya video za ngono inayoitwa Hot Shots kwa Kenrin ili kukwepa uchunguzi chini ya sheria ya India.

Programu hiyo ilipatikana kwenye Apple store na Google Play - zote ziliiondoa mwaka jana baada ya kupokea malalamiko.

"Ingawa kampuni ya Kenrin iko London, uundaji wa yaliyomo, shughuli na uhasibu vinashughulikiwa na kampuni ya Bwana Kundra iitwayo Viaan", amesema Bwana Bharambe.

BBC haijaweza kuwasiliana na kampuni ya Viaan ili kutoa maoni yao.

Jumanne, wachunguzi walisaka ofisi ya Viaan huko Mumbai na kupata filamu za ponografia.

Mazungumzo ya Whatsapp, barua pepe na karatasi za uhasibu za biashara hiyo pia zilikamatwa.

Hata hivyo, sio mara ya kwanza kwa Bwana Kundra kupatikana kwenye sakata.

Mnamo mwaka 2013, Bwana Kundra alikabiliwa na madai ya upangaji wa matokeo wakati wa mashindano ya Ligi Kuu ya Kriketi ya India.