Mfahamu mwanamke aliyetembea kwa miguu kuzunguka dunia

Angela Maxwell

Chanzo cha picha, Angela Maxwell

Kutafuta kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na dunia, Angela Maxwell alianza safari peke yake.

Miaka sita na kutembea umbali wa maili 20,000, baadaye akafanikiwa kuleta uhusiano huo nyumbani.

"Kwanini?"

Ni swali rahisi, na ambalo watu humuuliza Angela Maxwell mara kwa mara.

Hata hivyo hadi hivi majuzi, Mmarekani huyo alijitahidi kujibu, kwanini, haswa, alipoamua kuishi maisha mazuri kabisa kwa kutimiza ndoto yake hiyo kubwa.

Lakini kwa Maxwell, "kwanini? ni swali linalofaa kujibiwa.

Na baada ya yote, alianza safari ambayo watu wachache sana wanaweza kuijaribu: mnamo 2013, aliamua kutembea kote duniani - peke yake.

Chanzo cha picha, Angela Maxwell

Kutembea peke yako kwa umbali huu haikuwa kitu ambacho Maxwell alikuwa amepanga.

Na ukweli ni kwamba, aliondoka miezi tisa tu baada ya kusikia mazungumzo katika darasa lake la sanaa juu ya mtu ambaye inasemekana alitembea kote ulimwenguni.

Safari ya Maxwell haikuanzia mahali pa kupoteza, kushindwa au shida ya kibinafsi.

Alipoamua kuanza matembezi ya umbali mrefu, alikuwa katika miaka ya awali ya 30, akiwa anaendesha biashara iliyofanikiwa na alikuwa kwenye uhusiano.

"Nilidhani nilikuwa na furaha", alisema, lakini kwa kutazama tena, niligundua kuwa nilikuwa nikitafuta zaidi… uhusiano wa karibu zaidi na uasilia na watu kwa kuishi kuunganisha dunia na mimi.

Njia bora ya kufanikiwa katika hilo, alidhani, ilikuwa kwa kuweka mguu mmoja mbele ya mwingine.

Kutembea tena kwa kasi ndogo kulimaanisha kwamba angeweza kabisa kujiunganisha na uasilia, kukutana na watu ambao angeweza tu kiwapita katika hali ya kawaida, na kujua tamaduni zingine kwa njia ambayo ni ya kipekee kwa watembeao umbali mrefu.

Chanzo cha picha, Angela Maxwell

Alipokuwa akijiandaa, Maxwell alikutana na ulimwengu wote wa watafutaji wanawake ili kumtia ujasiri.

Alipenda uandishi na mtindo wa kusafiri polepole wa Robyn Davidson, ambaye alipitia Australia kwa kutumia ngamia.

Alijifunza juu ya mtembezi ya masafa marefu ya Ffyona Campbell, na kusoma juu ya Rosie Swale-Pope, ambaye alipanda baiskeli kutoka Ulaya hadi Nepal, akasafiri kote ulimwenguni, akavuka Chile akiwa amepanda farasi na, akiwa na umri wa miaka 59, akaanza kutembea kote ulimwenguni.

"Nilisoma vitabu vyao kwa matumaini ya kupata faraja - na nilifanya hivyo - kwa kujifunza juu ya changamoto zao na mapambano yao na ushindi wao".

"Hadithi ya kila mwanamke ilikuwa tofauti sana na ilinipa ujasiri wa kujaribu matembezi yangu", Maxwell alisema.

Mara tu alipofanya uamuzi wa kuanza kutembea, Maxwell aliuza mali zake zote na akapanga vitu muhimu alivyohitaji.

Alipakia mkokoteni na kilo 50 za vifaa vya kambini, chakula cha kuongeza maji mwilini, chujio ya maji inayotumiwa jeshini na nguo unazoweza kuvaa kwa misimu yote minnne.

Maxwell aliondoka katika mji wake wa Bend, Oregon, mnamo Mei 2, 2014 na kuanza safari yake na labda ilikuwa vizuri zaidi kutojua kilichokuwa kinamsubiri safarini.

Mara ya kwanza nina ungana na Maxwell kupitia Skype mnamo Juni 2018, tayari alikuwa karibu ana maliza miaka minne katika safari yake, akiwa ametembea zaidi ya maili 12,500 katika nchi 12 kwenye mabara matatu.

Kwa hamu, nilimuuliza ni aina gani ya mtu anahitajika kutembea kuzunguka ulimwengu.

Uso wake ukiwa unangaa, alitania, "mkaidi".

Kisha akaongeza, "Labda mchanganyiko wa tamaa, ukaidi kidogo na shauku - sio kwa kutembea kama mchezo, lakini kwa ugunduzi wa kibinafsi na utalii".

Maxwell aliniambia kuwa ingawa alipata kawaida yake ya utaratibu haraka - kuamka karibu na kuchomoza kwa jua, kunywa vikombe viwili vya kahawa na bakuli la oatmeal kwa kiamsha kinywa, kupakia vitu vyake na kuanza kutembea, kuweka kambi usiku unapoingia, kula tambi za papo hapo na kuingia ndani ya begi la kulala - hakuna siku iliyokuwa inafanana na nyengine.

Hapo awali, alianza kwa kuwa na mpango, lakini aligundua upotovu.

Ndio sababu, licha ya kufuata mwelekeo wa jumla, kila wakati angeamini hisia zake kila anapokwenda.

Maxwell aliugua malengelenge ya kuchomwa na jua na homa kali katika jangwa la Australia na homa ya dengue huko Vietnam.

Angeshambuliwa na kubakwa na wahamaji ambao walimvamia kwenye hema lake huko Mongolia.

Pia alikuwa anasikia milio ya risasi wakati amepiga kambi huko Uturuki na kujifunza kulala jicho moja na sikio moja likiwa wazi, na kuanza kuwa katika hatari ya usingizi mzito wakati wa mchana.

Ingawa haikuwezekana kujua kipi kitakuwa changamoto, Maxwell alikuwa ametarajia ugumu wa kila aina.

"Bado", alisema, "sikuanza kutembea kwasababu niliogopa. Niliogopa zaidi kutofuata moyo wangu kuliko kupoteza kila kitu nilichomiliki na kupenda".

Kukabiliana na mfadhaiko wa unyanyasaji wa kijinsia iligeuka kuwa wakati wa mabadiliko ambao Maxwell hatimaye aliamua kuendelea kutembea.

Wakati alikuwa bado anaogopa, hadithi zingine za wanawake za uvumilivu na nguvu zilimsaidia kuendelea.

"Nilidhamiria kutoruhusu tukio hilo kuwa sababu ya kutotimiza ndoto yangu hii na kurudi nyumbani. Nilikuwa nimeuacha ulimwengu wangu wote nyuma, sikuwa na chochote cha kurudia nyuma na nilielewa hatari zilizopo katika safari yangu".

Maxwell alikuwa akitembea kugundua jinsi anavyoweza kuwa hodari wa akili na mwili, hata wakati anakabiliwa na vurugu.

Njiani, kasi yake ndogo ilimruhusu kuvutwa - kwa kifupi lakini kwa undani - na tamaduni zingine.

Alizunguka vijiji vidogo kando ya Bahari ya Tyrrhenian huko Italia, katika mazingira mazuri na kukubali mwaliko wa mazungumzo, kukaa na kunywa divai.

Huko Vietnam, akiwa amechoka baada ya kufika kilele cha Hai Van Pass, alilakiwa na mwanamke mzee ambaye alimwalika kupumzika katika kibanda chake kidogo cha mbao kwa usiku.

Urafiki mmoja uliongezeka katika mpaka kati ya Mongolia na Urusi na kuwa chanzo cha kukutana tena miaka kadhaa baadaye huko Uswizi.

Maxwell hata alikua mama wa ubatizo kwa binti ya mwanamke ambaye alikutana naye nchini Italia.

Ikiwa mikutano hii ya kitamaduni ilidumu dakika saba au siku saba, Maxwell kila wakati aliweka mambo mawili akilini.

Kwanza, kuwa msikilizaji mzuri ili ujifunze.

"Kutembea kumenifundisha kuwa kila kitu na kila mtu ana hadithi ya kushirikisha wengine, kinachohitajika na kuwa na utayari wa kusikiliza", alisema.

Wakati wa safari yake, alijifunza mapishi ya familia ya kizazi cha zamani katika kijiji cha Italia, ufugaji nyuki katika Jamhuri ya Georgia na utunzaji wa ngamia huko Mongolia kwenye Barabara ya Hariri ya kihistoria.

Pili, Maxwell alijifunza umuhimu wa kutoa mchango.

Alikata kuni huko New Zealand na akawapatia chakula watu wasio na makazi nchini Italia.

Huko Sardinia, alimsaidia mkulima wa Italia kukarabati nyumba yake.

Mara nyingi zaidi kuliko hivyo, hadithi za Maxwell zilikuwa na mchango mkubwa katika jamii.

Alizungumza kwenye mikusanyiko isiyo rasmi, shule na vyuo vikuu, na hata kwenye majukwaa ya TEDx huko Edinburgh, akishirikisha wengine uzoefu wake kuwahamasisha.

Alikuwa sauti ya kuwawezesha wanawake, haswa baada ya kuamua kuendelea kutembea licha ya kushambuliwa huko Mongolia.

"Kuachana na ndoto yangu kamwe haikuwa chaguo", alisema.

Chanzo cha picha, Angela Maxwell

Wakati wote wa hija yake, Maxwell alikusanya michango kwa mashirika yasio ya kiserikali kama vile World Pulse na Her Future Coalition ambayo yanazingatia kusaidia wasichana na wanawake wadogo.

Kwa jumla, alikusanya karibu $ 30,000.

Kukubali udadisi na nia ya wazi, Maxwell alisema, ni njia nzuri ya "kufahamu zaidi ulimwengu na wakaazi wake.

Kwa miaka sita na nusu, Maxwell alichagua mtindo wa maisha wa udadisi, kutokuwa na uhakika na kuwa katika hatari kubwa.

Na alifanya hivyo akitafuta kitu ambacho hakuweza kuwa na uhakika wa kukipata: furaha ya kibinafsi na uunganisho zaidi na ulimwengu unaomzunguka.

Mnamo Desemba 16, 2020, hija ya Maxwell iliishia pale ilipoanzia: nyumbani kwa rafiki yake wa karibu Elyse huko Bend.

Kama tu alipokuwa anajibu wito wa kuanza safari yake, alijua ni wakati muafaka kuimaliza safari.

Alijua pia, kwamba hii safari yake imekuwa njia ya kuishi ambayo angeweza kuirudia wakati wowote ule.

Kwa sasa, hata hivyo, anafanya kazi kunapouzwa kitabu, akipanga safari za baadaye na kutengeneza njia za wanawake kupata, kuelezea na kuonyesha ujasiri katika maisha yao ya kila siku.

Ikiwa matembezi yanakuongoza nusu ya ulimwengu au chini tu ya barabara, Maxwell ameonyesha thamani ya kweli ya kupunguza kasi, kuzingatia zaidi na kutoa zaidi ya tunayopokea kadiri tunavyoendelea kuishi.