Rwanda yaondoa marufuku ya kutoka nje, mikusanyiko bado yapigwa marufuku

Serikali ilitoa mgao wa chakula kwa wasiojiweza waliokuwa majumbani

Rwanda imeondoa marufuku ya kutoka nje katika mji mkuu Kigali na wilaya nyingine 10 za nchi hiyo siku 15 baada ya kuweka marufuku hiyo katika kudhibiti ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona.

Kikao cha baraza la mawaziri jana usiku kilitangaza kuondoa marufuku hiyo kuanzia kesho juamapili na kwamba safari za kutoka mjini Kigali hadi mikoa mingine zimefunguliwa tena.

Kadhalika shughuli za utalii wa ndani,Hoteli na migahawa vimeruhusiwa kuendelea lakini migahawa imetakiwa kutayarisha chakula cha kupeleka nyumbani (Take away).

Bado shughuli za mikusanyiko ya Umma kama ibada ,michezo na burudani zitasalia kufungwa.ndoa zimeruhusiwa lakini kwa kuhudhuriwa na watu 10 tu.

Ni uamuzi uliopokelewa kwa shangwe na wakazi wengi wa mjini Kigali wakisema wiki mbili za kusalia nyumbani zilikuwa nyingi.

Serikali ilitoa mgao wa chakula kwa wasiojiweza na wanaoishi kwa kufanya kazi za vibarua ambazo zilisimamishwa katika mji wa Kigali na katika wilaya 10 zilizokuwa chini ya marufuku ya kutoka nyumbani.

Hata hivyo baadhi ya wananchi walisikika wakilalamika kutopata chakula hicho.

Tangu mwezi wa 6 hali ya maambukizi ilikuwa ya kutisha nchini Rwanda.Takwimu za wizara ya afya ya Rwanda zilionesha kwamba idadi ya maambukizi kwa siku ilikuwa kwa wastani wa watu 800 na vifo vya watu wasiopungua 10 kila siku kati ya mwezi wa 6 na mwezi wa 7.

Aina mpya ya kirusi cha Covid-19 chapatikana

Kulingana na wizara ya afya ,siku hizo 10 za mwanzo za marufuku ya kutoka nje zilisaidia kufanya vipimo kwa watu wengi na kusaidia wanaougua Covid wakiwa majumbani kwao.

Vipimo vilivyofanywa kwa wagonjwa 242 wa Covid,wiki iliyopita ,wizara ya afya ilitangaza kwamba asilimia 56% walipatikana na kirusi cha Delta kilichopatikana kwa mara ya kwanza nchini India,huku asilimia 4% wakipatikana na kirusi kingine ambacho wizara ilisema 'hakijafahamika '.

Mnamo siku saba zilizopita Rwanda ilirekodi maambukizi 7510, idadi ya watu wote waliokufa hadi kufikia sasa ni 798,huku watu laki 452.435 wakiwa wameishapata chanjo ya Covid19.