Babu wa Loliondo anaripotiwa kuwa aliugua homa kali ya mapafu na kupata tatizo la upumuaji

Dawa iliyokuwa ikitengenezwa na Babu wa Loliondo ikiwa kwenye vikombe

Chanzo cha kifo cha Mchungaji Ambilikile Mwasapile (86) kimetajwa aliugua homa kali ya mapafu ambayo ilimsababisha kupata tatizo la upumuaji na homa. Gazeti la Mwananchi limeripoti

Tangu afariki wasaidizi wake na majirani wamekuwa wakieleza kushtushwa na kifo hicho ambacho kimetokea akiwa anaendelea kutoa huduma ya tiba ya kikombe aliyoanza tangu mwaka 2011.

Mchungaji Ambilikile ambaye ataendelea kukumbukwa kwa kuvutia maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kati ya mwaka 2011 hadi 2013 kutokana na tiba yake ya kikombe alifariki jana saa 9:45 jioni.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala alinukuliwa na Mwananchi akisema kuwa taarifa za awali za madaktari zinaeleza chanzo cha kifo ni homa ya mapafu ambapo kwa takriban siku tano alikuwa anaumwa na kupata sindano za saa.

"Jana asubuhi aliamka vizuri akiendelea na matibabu lakini majira ya saa nane alianza kujisikia vibaya ndipo ilitafutwa gari kutaka kumpeleka hospitali ya Wasso ambaye alitaka,"

Hata hivyo amesema wakiwa wanampandisha gari alijisikia vibaya na kuanza kutapika ndipo walipomkimbiza kituo cha afya Chadigodigo na alifika akiwa tayari amefariki.

Baadhi ya wasaidizi wa mchungaji Mwasapile walisema kabla ya kuzidiwa na ugonjwa alikuwa akiendelea kutoa tiba ya kikombe kwa wagonjwa kadhaa wakiwemo wa corona.

"Wiki mbili zilizopita alikuwa vizuri anatoa tiba japo kwa watu mmoja mmoja waliokuwa wanakuja lakini hali yake iliendelea kubadilika."