Muigizaji gwiji wa filamu Nigeria Rachel Oniga aaga dunia kwa matatizo ya moyo

Muigizaji gwiji wa filamu za Nollywood nchini Nigeria Rachel Oniga

Chanzo cha picha, ONIGA/TWITTER

Muigizaji gwiji wa filamu za Nollywood nchini Nigeria Rachel Oniga ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64.

Familia yake imetoa taarifa ikisema kuwa Rachel aliaga dunia Ijumaa akiwa hospitalini alikokuwa akipatiwa matibabu ya moyo , na kutupilia mbali madai kuwa alipoteza maisha baada ya kuugua Covid-19.

Familia imesema ''ingawa ni huzuni kubwa tumepokea kwa imani na heshima kubwa kwa Mwenyezi Mungu.''

Familia ya Rachel imetaka kupatiwa nafasi ya kuomboleza kifo cha Rachel na kuwa muda mfupi ujao watatoa taarifa za mipango ya mazishi.

Marehemu Bi. Oniga alizaliwa tarehe 23 mwezi Mei mwaka 1957 na alianza kazi ya uigizaji mwaka 1993.

Waigizaji mbalimbali wamemuomboleza na kutoa salamu za rambirambi kwa familia na tasnia ya filamu

Oniga mzaliwa wa jimbo la Delta amecheza filamu nyingi zilizopendwa sana Nigeria na nje ya nchi hiyo kama vile Chief Daddy, Super Story na Onome.

Kifo cha muigizaji huyu kimekuja wakati ambapo tasnia ya burudani nchini humo likiwa bado linamuomboleza muimbaji maarufu Sound Sultan.

Chanzo cha picha, ONIGA

Maelezo ya picha,

Moja ya filamu za hivi karibuni 'My Village' iliyotoka mwezi Juni mwaka 2021

Olanrewaju Ganiu Fasasi maarufu Sound Sultan alipoteza maisha tarehe 11 mwezi Julai mwaka 2021 kwa saratani ya mapafu.