Mashindano ya Olimpiki Tokyo: Mwanariadha wa Namibia anasema 'huwezi kuniambia kwamba mimi sio mwanamke'

Mwanariadha wa Namibia Beatrice Masilingi akiwa katika mashindano ya olimpiki mjini Tokyo

Chanzo cha picha, Henk Botha

Maelezo ya picha,

Mwanariadha wa Namibia Beatrice Masilingi akiwa katika mashindano ya olimpiki mjini Tokyo

Mwanariadha wa Namibia Beatrice Masilingi anajiandaa kushiriki katika mashindano makubwa duniani.

Beatrice mwenye umri wa miaka 18 anasema kwamba anafurahia kushiriki katika mbio za mita 200 upande wa akina dada katika mashindano ya Olimpiki ya 2020 yanayofanyika mjini Tokyo ambapo mbio za kufuzu kwa fainali zitaanza siku ya Jumatatu.

Lakini mbio hizo ni chaguo lake la pili na alikuwa anajiandaa kushiriki mbio za mita 400 ambapo alikuwa miongoni mwa wanariadha wanaopigiwa upatu baada ya kuweka muda bora zaidi mwaka huu wa sekunde 49.53.

Furaha yake katika mashindano ya kufuzu kwa Olimpiki hatahivyo ilikatizwa wakati alipoambiwa na shirikisho la riadha duniani kwamba hangeweza kushiriki katika mbio za mita 400 katika michezo hiyo kutokana na kuwa na viwango vya juu vya homoni za kiume mwilini.

"Mwanzo nilijihisi vibaya sana , huwezi kuja kuniambia kwamba sasa mimi sio mwanamke. Inakera sana lakini hakuna kitu ninachoweza kufanya kwa sasa'', aliambia BBC Sport Afrika.

''Inakatiza tamaa, na inakasirisha pia, nilikuwa najiandaa kushiriki katika mashindano ya Diamond League wakati nilipoona habari hizo''.

''Kwa kweli sio haki kwasababu huwezi kutaraji watu watafanana, kila mtu kuwa na uwezo sawa, tumezaliwa na uwezo tofauti , hatuwezi kuwa sawa , haileti maana''.

Masilingi alielezwa mwezi Julai na shirikisho la riadha duniani kwamba viwango vyake vya homoni za testosterone vilikuwa zaidi ya viwango vilivyoruhusiwa miongoni mwa wanariadha wanawake wanaotaka kushiriki katika mbio za mita 400 hadi maili moja, la sivyo wapunguze viwango vyao vya testosterone kwa muda usio chini ya miezi sita.

Licha ya kukatizwa tamaa , kijana huyo yuko tayari kufurahia uwepo wake katika michezo hiyo.

''Nafurahia sana ni mojwapo ya malengo yangu makuu , lakini sikudhania kwamba ningeweza kufaulu nikiwa na umri huu'', Masilingi aliambia BBCSport Afrika.

Maelezo ya picha,

Mwanariadha wa Namibia Christine Mboma ambaye alivunja rekodi ya vijana ya mita 400 mapema mwaka huu hatoruhusiwa kushiriki

Namibian teenager Christine Mboma - who broke the World 400m Under-20s record this year - won't be allowed to run the event at the Olympics

Ili kuweza kuimarisha ndoto yake zaidi, Masilingi na mshirika wake wa mazoezi Christine Mboma , ambaye pia aliathiriwa na sheria hizo aliamua kubadili mpango wao wa mazoezi na kujiandaa kwa mbio za mita 200 wiki chache kabla ya mashindano hayo.

"Ukweli ni kwamba hatua hiyo imeturudisha nyuma sana . Tulilazimika kubadili na kujaribu uwezo wetu na sasa najivunia wasichana hawa wawili jinsi wanavyojifunza'', alisema mkufunzi wa wanariadha hao wawili Henk Botha..

Masilingi anakataa kuweka malengo katika michezo hii , lakini anasema kwamba anafurahia kwamba atashiriki licha ya kukatizwa tamaa hapo awali..

"Nadhani nina fursa nyengine , nina mbio za mita 200 ambazo naweza kushiriki, hivyobasi sitaki kuvunjika moyo kwasbabau ya mbio ambazo nimeambiwa siwezi kushiriki. Bado naweza kuwa na furaha kama ile niliokuwa nayo katika mbio za mita 400," alisema..

"Najaribu kutokuwa mwingi katika mitandao ya kijamii kwasababu najua hilo litanileta presha na najaribu kuzuia kila kitu kwasababu sina uzoefu wa kutosha."