Bobi Wine: Mfahamu mwanasiasa mwiba anayeikosesha usingizi serikali ya rais Museveni Uganda

Bobi Wine

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bobi Wine

Katika mfululizo wa Makala ya wiki hii tunawaangazia wanasiasa ambao wamekuwa mwiba kwa serikali zilizopo madarakani katika eneo la Afrika mashariki na jinsi wanavyoziwajibisha serikali hizo.

Baadhi ya wanasiasa ni maafisa wa serikali wanaopigana dhidi ya serikali hizo kutoka ndani.

Robert Kyagulanyi Ssentamu , maarufu kwa jina Bobi Wine ni kijana ambaye ni mwanasiasa , mwanaharakati, mwimbaji , muigizaji na mfanyabiashara.

Robert Kyagulanyi alizaliwa tarehe 12 mwezi Februari 1982 na kukulia katika mtaa wa mabanda wa Kamyookya kaskazini mashariki mwa Kampala.

Alijiunga na shule ya msingi ya Kitante Hill School, ambapo alipata cheti cha shule ya msingi 1996.

Baadaye alielekea katika shule ya sekondari ya Kololo Senior Secondary School na kumaliza mwaka 1998.

Bobi alijiunga na chuo kikuu cha Makerere mjini kampala , ambapo alijifunza muziki na uigizaji kabla ya kuhitimu masomo yake ya ngazi ya Diploma mnamo mwaka 2003.

Mwaka 2016 Bobi Wine alipata fursa ya kusomea shahada ya sheria katika chuo kikuu cha International University of East Africa (IUEA).

Kazi ya muziki ya Bobi Wine

Miaka 12 iliyopita, Bobi alikuwa akijulikana kwa kuimba nyimbo zinazoeleza maisha ya watu masikini - yeye mwenyewe akiwa amezaliwa na kukulia katika mazingira ya kimaskini huko Kamwokya, na hilo ndilo jambo lililompa umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi wa taifa hilo ambao wengi wao ni maskini.

Alianza kazi yake ya usanii wa muziki mapema miaka 2000 na kupatiwa Bobi Wine.

Muziki wake una miondoko ya Reggae, dance hall, na afrobeat, kila mara ukiwa na ujumbe wa kuamsha jamii.

Vibao vyake Akagoma, Funtula na Sunda vilimfanya kufanikiwa kati muziki wa Afrika Mashariki, kufikia sasa ameachilia zaidi ya nyimbo 70 katika kipindi cha miaka 15.

Alipojiunga na siasa

Bobi Wine alionesha hamu yake ya kutaka kuwania ubunge mwaka 2017 na kupata ushindi mkubwa dhidi ya wanasiasa wawili wakongwe.

Miaka miwili baadaye , alitangaza azma yake ya kuwania wadhfa wa urais katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2021 lakini alipoteza kwa rais aliyepo madarakani Yoweri kaguta Museveni.

Kwasasa ndiye kiongozi wa chama national Unity Platfform baada ya kuchaguliwa kama mgombea wa urais wa chama hicho.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jinsi Bobi Wine alivyotikisa siasa za Uganda

Bila kujali jinsi raia wa Uganda walivyopiga kura Januari 14, rais Museveni alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo uliokumbwa na visa vya kuzimwa kwa mtandao.

Museveni amelitawala taifa hilo kwa miula mitano mfululizo na sasa anahudumia muhula wake wa sita kama rais.

Lakini kipindi chote cha kampeni za uchaguzi wa 2021, Museveni alionekana kupata ushindani mkali kutoka kwa mwanamuziki huyo.

Tangu alipochaguliwa kuwa mbunge 2017, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 38 amekuwa sura mpya ya upinzani nchini Uganda.

Alianzisha vuguvugu kinyume na matarajio ya wengi

Bobi Wine mara kwa mara amepuuzwa na serikali pamoja na wakosoaji wake tangu alipowania ubunge.

Alilazimika kuwania kiti cha ubunge kama mgombea huru baada ya vyama viwili vikubwa vya upinzani kumkataa.

Hatahivyo alipata ushindi kwa urahisi katika eneo bunge la Kyadondo lililopo mjini Kampala akijipatia kura asilimia 78.

Tangu wakati huo, ameonesha kuwa mwanasiasa shupavu mwenye ujuzi ambaye amefanikiwa kuanzisha vuguvugu lenye uwezo mkubwa.

Katika miaka miwili ya kwanza ofisini , alijipatia sifa ya kuwa mtu anayefuata kanuni na asiyeogopa .Alikuwa sauti iliopinga kuondolewa kwa kikomo cha miaka ya urais katika katiba.

Pia aliongoza maandamano dhidi ya serikali kuongeza tozo katika mitandao ya kijamii mwezi Julai 2018.

Katika kipindi hicho aliwapendekeza wagombea wanne wa upinzani ambao wote walifanikiwa kupata ushindi katika maeneo bunge yao.

Kufikia 2018 , alianzisha kikundi kimoja kwa jina 'Peoples Power , Our Power'. Serikali ilipozuia usajili wake kama chama rasmi , Bobi Wine alijiunga na chama kidogo ambacho alikipatia jina la National Unity Platform.

Muda mfupi baadaye zaidi ya wabunge 20 walihama vyama vyao vya upinzani ili kujiunga na chama chake.

Alilengwa na ukandamizaji wa serikali

Bobi Wine amekuwa akilengwa na ukandamizaji wa serikali.

Utawala wa rais Museveni ulijibu mafanikio yake kwa kumzuia kutofanya matamasha na kupiga marufuku umma kutovaa kofia nyekundu ambazo zilishirikishwa na nembo ya Peoples power.

Tangu alipochaguliwa , Bobi Wine hajapatikana na hatia yoyote . Baadhi ya wafuasi wa vuguvugu lake wameauwa na mara nyingine kwa njia ya shauku.

Wengi wamekamatwa . Wakati mmoja mwezi Agosti 2018 , alipokuwa akimfanyia kampeni mgombea mwenza wa chama huru katika uchaguzi mdogo wa Arua kaskazini magharibi mwa Uganda , Bobi Wine na takriban wafuasi wake 35 walikamatwa kufuatia ripoti kwamba msafara wa rais Museveni ulipigwa mawe.

Usiku huohuo , dereva wa kiongozi huyo wa upinzani Yasin Kawuma, aliuawa baada ya kupigwa risasi ambayo Bobi Wine anaamini kwamba ilimlenga yeye.

Baada ya kukamatwa, mbunge huyo wa kyadondo mashariki alishtakiwa kwa uhaini na kumiliki silaha .

Katika kipindi cha siku kumi alichokuwa gerezani , alipigwa vibaya na maafisa wa usalama wa serikali, hatua iliomfanya kushindwa kutembea. Hatahivyo alitafuta matibabu nchini Marekani ili kuuguza majeraha aliopata.

Licha ya jamii ya kimataifa kulalamikia hatua hiyo, tukio hilo halikuuzuia utawala wa rais Museveni kutotumia njia zake za ukandamizi wakati wa uchaguzi uliopita.

Chanzo cha picha, Reuters

Kamatakamata iliendelea bila wasiwasi katika kipindi chote . Kwa kuongeza, mikutano ya kampeni iliwekwa masharti na serikali iliwakabili wafuasi wa upinzani kwa kutumia nguvu mara kadhaa.

Cha kusikitisha zaidi, kufuatia kukamatwa kwa Bobi Wine katikati ya mwezi Novemba, maandamano ya kitaifa yalizuka wakati ambapo watu wasiopungua 54 waliuawa.

Kujibu unyanyasaji huo, mapema mwezi Januari, Bobi Wine na wengine wawili waliwasilisha malalamiko ya kurasa 47 katika mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa dhidi ya Museveni na maafisa tisa wa usalama wa serikali yake, wakiwatuhumu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu tangu 2018 .

Bobi Wine na ushawishi kwa vijana

Amebuni harakati zake za kisiasa kwa maneno ya kizazi: "kizazi cha Facebook", ambacho anawakilisha dhidi ya "masilahi yaliyojikita mizizi ya" kizazi cha utawala wa Museveni.

Ameweza kuzungumza na - na kuelezea - hisia kali za hasira na malalamiko ambayo vijana wa Uganda wanahisi kuhusu utawala wa Museveni.

Kwa kufanya hivyo, "Rais huyo wa Ghetto" wa Uganda amekuja kuwa uso na sauti ya vijana.

Maelezo ya video,

Mtanzania atengeneza jiko la umeme linalotumia mawe