Mzozo wa Msumbiji: Majeshi ya Rwanda yateka ngome ya wanamgambo Msumbiji

Rwanda yaongoza majeshi yake kukabiliana na wapiganaji Msumbiji

Chanzo cha picha, Reuters

Wanajeshi wa Rwanda wanaopigana na wanamgambo wa kijihadi nchini Msumbiji wafanikiwa kuukomboa mji wa bandari wa Mocimboa da Praia. Mji huo umekuwa ngome ya wanamgambo kwa mwaka mmoja.

Nchi za Jumuia ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika pia zimeanza kupeleka wanajeshi kaskazini mwa Msumbiji kusaidia vikosi vya serikali ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na wakati mgumu kudhibiti wavamizi hao.

Zaidi ya watu 800,000 wametoroka makwao kufuatia mzozo ambao umelikumba taifa hilo la Afrika lenye hifadhi kubwa ya gesi .

Hatua hiyo ni ushindi kwa serikali ya Msumbiji baada ya kushindwa vibaya katika miaka ya hivi karibuni. Lakini sifa zaidi zinaendea majeshi wa Rwanda ambao wamekuwa nchini humo tangu mwezi uliopita.

Mocimboa da Praia inachukuliwa kuwa makao makuu ya kidini ya wanamgambo wa al-shabab - shambulio lao kuu la kwanza lilikuwa kwenye mji huo mnamo 2017 - kabla ya kuendelea kuudhibiti mnamo 2020. Pia imewapa kituo cha kuwahifadhi wapiganaji na vifaa vya duka.

Uhusiano 'dhaifu' na IS

Waasi wanaitwa "al-Shabab", jina ambalo kwa kienyeji linamaanisha "vijana" na halina uhusiano na kundi lenye jina sawa na hilo nchini Somalia.

Eneo lenye mzozo linakaliwa na Waislamu wengi, na kufikia mwaka 2019 waasi walikuwa wamewasiliana na kundi la Islamic State (IS).

Marekani imewapatia jina la "Isis Mozambique" na kuwataja kama shirika la kigeni la ugaidi.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Watu wengi hutegemea uvuvi kujikimu kimaisha kaskazini mwa Msumbiji.

Wakati vikosi vya Rwanda vikiwa vimeanza mashambulia dhidi ya waasi, wachambuzi wanasema kundi hilo limegawanyika katika vitengo vidogo, ambayo vinaweza kuwa ngumu kupigana.

Sehemu kubwa ya maeneo karibu na miji kama Mocimboa da Praia imezungukwa na mIsitu mIkubwa ambayo ni maeneo bora zaidi ya kujifika ya wapiganaji.