Vita vya Afghanistan: Je, ni nani walio kwenye utawala wa Taliban?

Mawlawi Hibatullah Akhundzada ni kiongozi wa kisiasa na kidini ambaye ni Kamanda Mkuu wa tatu wa Taliban

Chanzo cha picha, Getty Images

Kundi la wapiganaji wa Taliban liliwashangaza wengi kwa kufanikiwa kuiteka nchi hiyo ndani ya siku kumi pekee. Na kuchukua kwa kasi miji na miji mikuu. Bado haijulikani ni nani atakayechukua uongozi wa serikali mpya . lakini ni kipi tunachojua kuhusu uongozi wa kundi hilo?

1. Hibatullah Akhundzada

Hibatullah Akhundzadandiye aliyechukua uongozi wa kundi hilo mwezi Mezi 2016. Miaka ya 80 , alishiriki katika vita vya kundi hilo dhidi ya jwshi la Usovieti nchini Afghanistan , lakini sifa yake ni zaidi ya ile ya kiongozi kidini badala ya kamnada wa jeshi la Taliban.

Akhundzada alifanya kazi kama mkuu wa mahakama za sharia katika miaka ya tisini. Baada ya kuchukua mamlaka miaka ya tisini , Kundi la taliban lilianzisha na kuunga mkono adhabu kulingana na sheria za Kiislamu : Waliuawa hadharani wauaji na wazinzi na kjuwakata mikono wezi.

Chini ya uongozi wa Mullah Mohammed Omar ambaye anafikiriwa kufariki 2013 , Taliban walipiga marufuku runinga, muziki, filamu, vipodozi na kuwazuia wasichana walio na umri wa miaka 10 na zaidi kwenda shule.

Chanzo cha picha, EPA

Akhundzada anaaminika kuwa katika miaka yake ya sitini na ameishi Maisha yake mengi nchini Afghanistan, hatahivyo kulingana na wataalamu , ana uhusiano wa karibu

Hatahivyo, kulingana na wataalam, ana uhusiano wa karibu na kile kinachoitwa "Quetta Shura" - viongozi wa Taliban wa Afghanistan wanaosemekana wako katika mji wa Quetta nchini Pakistani.

Kama kamanda mkuu wa kikundi hicho, Akhundzada ndiye anayesimamia masuala ya kisiasa, jeshi na dini.

2. Abdul Ghani Baradar

Chanzo cha picha, Getty Images

Mullah Abdul Ghani Baradar ni mmoja wa watu wanne ambao walianzisha Taliban huko Afghanistan mnamo 1994.

Alikamatwa katika operesheni ya pamoja ya Marekani na Pakistani katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistani mnamo Februari 2010.

Alikaa gerezani kwa miaka minane, hadi alipoachiliwa kama sehemu ya mpango wa kuwezesha mchakato wa amani. Amekuwa mkuu wa ofisi yao ya kisiasa nchini Qatar tangu Januari 2019.

Mnamo 2020, Baradar alikua kiongozi wa kwanza wa Taliban kuwasiliana moja kwa moja na rais wa Marekani baada ya kufanya mazungumzo ya simu na Donald Trump.

Leo, Abdul Ghani Baradar ndiye kiongozi mkuu wa kisiasa wa Taliban.

"Tumefanikiwa ushindi ambao haukutarajiwa ... sasa inahusu jinsi tunavyowahudumia na kuwalinda watu wetu," Baradar alisema katika taarifa iliyoandikwa huko Doha, mji mkuu wa Qatar, ambapo alikuwa sehemu ya timu ya mazungumzo ya Taliban ya mazungumzo ya amani.

Chanzo cha picha, Getty Images

3. Mohammad Yaqoob

Anaaminika kuwa na zaidi ya miaka 30 na kwa sasa ndiye kiongozi wa operesheni za jeshi la kikundi hicho.

Baada ya kifo cha kiongozi wa zamani wa Taliban Akhtar Mansour mnamo mwaka 2016, wanamgambo wengine walitaka kumteua Yaqoob kuwa kamanda mkuu wa kikundi hicho, lakini wengine walihisi kuwa alikuwa mdogo na hana uzoefu.

Kulingana na vyombo vya habari vya huko, Yaqoob anaishi Afghanistan.

4. Sirajuddin Haqqani

Sirajuddin Haqqani ni mmoja wa manaibu viongozi wakuu wa kikundi.

Baada ya kifo cha baba yake, Jalaluddin Haqqani, alikua kiongozi mpya wa mtandao wa Haqqani, ambao umetajwa kuwa na mashambulio makali zaidi ambayo yametokea Afghanistan dhidi ya vikosi vya Afghanistan na washirika wao wa Magharibi miaka ya hivi karibuni.

Mtandao wa Haqqani kwa sasa ni moja ya vikundi vya wanamgambo vyenye nguvu na wanaoogopwa. Wengine wanasema lina ushawishi zaidi kuliko kundi la Islamic State huko Afghanistan.

Chanzo cha picha, FBI

Haqqani anaaminika kuwa na umri wa miaka 45 na haijulikani alipo.

5. Abdul Hakeem

Mnamo Septemba 2020, Taliban ilimteua Abdul Hakeem kama mkuu mpya wa timu ya mazungumzo ya Taliban huko Doha.

Anaaminika kuwa na umri wa miaka 60. Aliripotiwa kuendesha madrassa - shule ya dini ya Kiislamu - huko Quetta, Pakistan, ambapo pia alisimamia mahakama ya Taliban.

Viongozi wengi waandamizi wa Taliban waliripotiwa kukimbilia Quetta, ambapo waliongoza kikundi hicho.

Lakini Islamabad imekanusha uwepo wa "Quetta Shura".

Hakeem pia anaongoza baraza lenye nguvu la wasomi wa dini la Taliban na anaaminika kuwa mmoja wa watu wa karibu na kamanda mkuu, Akhundzada.