Maharage ya Jesca: Tiba ya nguvu za kiume, kisukari-Watafiti

Maharage ya Jesca hayatumiwi kwa mtu au jinsi moja isipokuwa hata watoto wanaweza kutumia ili kuwafanya kukua kiafya na kiakili na kwamba inaongeza pia damu

Chanzo cha picha, Mwananchi

Kituo cha Utafiti Uyole (Tari) kimesema zao la maharage aina ya Jesca licha ya kuongeza nguvu za kiume lina faida zaidi kwa binadamu kwakuwa linatibu matatizo mengi. Gazeti la Mwananchi limeandika

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera wakati alipofanya ziara katika Chuo cha Utafiti Uyole, amewataka wananchi kuacha matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume (Viagra)bali watumie maharage aina ya Jesca ili kumaliza tatizo na kulinda ndoa zao.

Jumamosi Mwananchi lilifika katika kituo cha utafiti Uyole, ambapo watafiti wa kituo hicho wameeleza matumizi na faida za Jesca kwa binadamu kiafya na kiuchumi.

Dk Michael Kilango amesema zao hilo lina faida nyingi zikiwemo kuboresha njia za uzazi, matatizo ya uzazi, magonjwa ya kisukari, mafua na kuongeza kinga za mwili kutokana na madini iliyonayo ya Zinc na chuma na kwamba hata kwa wakulima ni faida kwani yanastawi sehemu yoyote na yanakomaa haraka ndani ya miezi mitatu.

Amesema maharage ya Jesca hayatumiwi kwa mtu au jinsi moja isipokuwa hata watoto wanaweza kutumia ili kuwafanya kukua kiafya na kiakili na kwamba inaongeza pia damu.

"Baada ya kupimwa imebainika maharage aina ya Jesca yana madini ya zinki, chuma na vitamini kwa wingi ukilinganisha na maharage mengine ndio maana yamepata mwamko mwingi haswa kwa wenye matatizo ya damu na uzazi" Kilango aliiambia Mwananchi.

Kwa upande wake Aida Magelanga ambaye ni mtafiti wa maharage hasa Jesca, amesema tangu zao hilo litangazwe limekuwa na soko kubwa kwa wakulima na watumiaji na kwamba kwa siku wanapokea wateja zaidi ya kumi.

"Tumeona mwitikio kwa watu wengi, niwaombe waendelee kuitumia kwa chakula, dawa na kuboresha thamani kwa mazao mengine na kurutubisha miili yao" amesema Aida.

Naye Mkurugenzi wa TARI Uyole, ambaye ni daktari wa Filosofia na mbunifu wa mbegu za mazao, Tulole Lugendo amesema kutokana na uhitaji wa zao hilo wanatarajia kuzalisha tani tano kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

"Kwakuwa Serikali imetusaidia visima vya maji, tutakuwa tukimwagilia wakati wa kiangazi na mwaka huu tunatarajia kuzalisha tani tano ili kukidhi mahitaji ya wananchi" amesema Lugendo.