Gazeti la Raia Mwema lafungiwa kwa siku 30 nchini Tanzania

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari Gerson Msigwa

Chanzo cha picha, Msigwa/Twitter

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari Gerson Msigwa amesitisha kwa muda wa siku 30 leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Raia Mwema kuanzia kesho tarehe 6 mwezi Septemba mwaka 2021.

Uamuzi wa kusitisha leseni ya gazeti hilo unatokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari na makala ambao kwa kiasi kikubwaunakiuka misingiya maadili ya taaluma ya habari kwa kufanya upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa na uchochezi wa bayana, taarifa imeeleza.

Taarifa hiyo imesema kuwa kwa vitendo hivyo gazeti limekiuka masharti ya leseni iliyopewa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni wa jamii na vileile kuwafanya wanachi wachukie serikali na viongozi wake.

Mfano wa makala ambazo zinaelezwa kukiuka masharti ya leseni , misingi ya maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kiasi kikubwa ni pamoja na gazeti lililochapisha habari iliyokuwa na kichwa habari '' Maumivu mapya 17''.

Katika taarifa hiyo gazeti lilikwenda kinyume na vifungu 52(1) (a), (c), (d) na (e) pamoja na 54(1) vya sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya mwaka 2016, kwa kuchapisha na kusambaza habari zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na wananchi kuonesha kuwa serikali inawaletea maumivu wananchi kwa kuweka tozo 17 za kazi mbalimbali za wasanii.

Gazeti hilo pia liliandika habari yenye kichwa kisemacho ''Hamza wa CCM hatari''. Kwanza kwa kuonekana dhahiri kukosa weledi na udanganyifu, gazeti hili lililotolewa tarehe 3 Septemba, 2021 liliandikwa limetolewa tarehe 3 mwezi Agosti, 2021 na katika habari hiyo linawanukuu watu wawili lililowaita Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) Manumba, mara linamtaja DCI Wambura, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa gazeti hilo lilitaka kuuaminisha Umma kuwa Hamza ni mwanachama wa CCM ama kiongozi wa CCM (Chama Tawala) bila kuwa na uthibitisho usioacha shaka yoyote jambo ambalo linaweza kuleta chuki miongoni mwa wanachama wa CCM na makundi mengine ya jamii.

Halikadhalika katika gazeti hilohilo iliandikwa habari yenye kichwa kisemacho 'DC kizimbani akidaiwa milioni 100'. Taarifa ya Mkurugenzi huyo imesema habari hiyo ilikosa weledi kwani kichwa cha habari hiyo hakikushabihiana na maudhui yaliyoandikwa katika habari hiyo kwa kuonesha kuwa DC anayezungumzwa yupo madarakani wakati mwandishi alijua kuwa anamzungumzia DC ambaye alikuwa ameshastaafu.

Taarifa imesema kuwa iwapo wahusika hawataridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara na Huduma za Habari, wanayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari ndani ya siku thelathini tangu siku ya uamuzi huo.