Mali:Polisi washambulia gereza na kumtorosha kamanda wao aliyekamatwa

vikosi maalumu vimepata mafunzo kutoka EU na Marekani kusaidia kupamana na makundi ya jihadi

Chanzo cha picha, AFP

Polisi wa kupambana na ugaidi nchini Mali wamelaaniwa sana baada ya maafisa wenye silaha kuandamana kwenda gerezani kutaka kuachiliwa kwa kamanda wao - ambaye aliachiliwa huru.

Mazingira ya jinsi Oumar Samake aliachiliwa haijulikani.

Ripoti zingine zinasema walinzi wa magereza waliondoka, wakati wengine wanasema serikali iliamuru aachiliwe kuepusha machafuko.

Kamanda Samake alishtakiwa kwa mauaji juu ya vifo vya waandamanaji wapatao 14 wanaopinga serikali mnamo Julai 2020.

Serikali ya mpito ya Mali ililaani kitendo hicho cha "watu waliovalia sare na wenye silaha" kutoka Kikosi Maalum cha Kupambana na Ugaidi (Forsat) katika taarifa ya Runinga, shirika la habari la AFP linaripoti.

Chama cha Haki za Binadamu cha Mali (AMDH) kilisema "kilishtuka sana" na kilitaja shambulio hilo kama shambulizi dhidi ya sheria

Ilisema maafisa walikuwa wamefyatua risasi katikati mwa mji mkuu, Bamako, Ijumaa kabla ya kuelekea kwenye gereza kuu la jiji, ambapo kamanda wa Forsat Samake alikuwa amezuiliwa masaa kadhaa mapema.

Kitengo hicho cha vikosi maalum kimepokea mafunzo kutoka kwa EU na Marekani kusaidia katika vita dhidi ya vikundi vya jihadi ambavyo vimekuwa vikifanya uasi kwa muda wa miaka kumi nchini Mali.

UN na Ufaransa zina maelfu ya walinda amani walioko huko kusaidia kukabiliana na wanajihadi.

Lakini machafuko hayo yameiacha nchi hiyo bila utulivu, na imeshuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi katika mwaka uliopita.