Afghanistan: Taliban washutumiwa kumuua polisi wa kike

Banu Negar

Chanzo cha picha, Family photo

Wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan wamemuua kwa kumpiga risasi polisi wa kike, mashuhuda wameiambia BBC.

Mwanamke huyo, aliyetajwa katika vyombo vya habari vya ndani kama Banu Negar, aliuawa nyumbani kwao mbele ya jamaa zake huko Firozkoh, mji mkuu wa mkoa wa kati wa Ghor.

Mauaji hayo yanatokea wakati ripoti zikizidi kuongezeka za ukandamizaji wa wanawake nchini Afghanistan.

BBC imewatafuta maafisa wa Taliban kujibu shutuma hizo. Taliban katika eneo hilo waliahidi kuchunguza, familia inasema.

Maelezo ya tukio hilo bado hayafahamiki kwani wengi huko Firozkoh wanaogopa kulipiza kisasi ikiwa watazungumza. Jamaa walitoa picha zinazoonesha damu iliyotapakaa ukutani kwenye kona ya chumba na mwili, uso ukiwa umeharibika sana.

Familia inasema Negar, ambaye alifanya kazi katika gereza la mkoa huo, alikuwa na ujauzito wa miezi minane.

Watu watatu wenye bunduki walifika nyumbani Jumamosi na kupekua kabla ya kuwafunga watu wa familia hiyo na kumpiga risasi mbele yao.

Wavamizi hao walisikika wakiongea Kiarabu, shuhuda alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images

Tangu wachukue madaraka tarehe 13 Agosti, Taliban imejaribu kujionyesha kama mvumilivu kuliko sifa yake, lakini visa vya ukatili na ukandamizaji bado vinaripotiwa katika sehemu za nchi.

Makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakirekodi mauaji ya kulipiza kisasi, kuwekwa kizuizini na kuteswa kwa watu. Taliban imesema rasmi kwamba haitalipa kisasi dhidi ya wale waliofanya kazi na serikali ya zamani.

Elimu ya wanawake ilipigwa marufuku chini ya kipindi cha zamani cha utawala wa Taliban miaka ya 1990, lakini sasa wametoa mwongozo juu ya ufundishaji katika vyuo vikuu.

Wanawake wataruhusiwa kuhudhuria, lakini madarasa yatatengwa kwa jinsia, na wanafunzi wa kike lazima wavae na abaya, au joho, na niqab, aukufunika uso, AFP limeripoti.

Siku ya Jumamosi, maafisa wa Taliban walivuruga maandamano ya wanawake kadhaa huko Kabul wakidai kuendelea kwa haki zilizojengwa tangu kumalizika kwa kipindi cha zamani cha Taliban madarakani.

Kundi hilo linasema kuwa Taliban iliwafurusha kwa mabomu ya machozi na dawa ya pilipili wakati walipojaribu kutembea kutoka darajani kwenda Ikulu ya rais.

Wakati huo huo, mapigano yanaripotiwa kuendelea katika Bonde la Panjshir, kaskazini mwa Kabul. Jimbo hilo ndilo sehemu pekee ya Afghanistan inayopinga utawala wa Taliban.

Taliban wanasema vikosi vyao sasa viko katika mji mkuu wa mkoa, Bazarak, ambapo walisababisha "majeruhi wengi".

Lakini chama cha upinzani cha National Resistance Front cha Afghanistan hapo awali kilishutumu Taliban kwa kueneza propaganda bandia.