Mapinduzi ya Guinea:Rais Alpha Condé akamatwa na jeshi linalodai kuchukua madaraka

Chanzo cha picha, GUINEA TV
Umoja wa Afrika umelaani mapinduzi nchini Guinea na kulitaka jeshi kumuachilia rais Alpha Conde mara moja Katika taarifa rais wa AU Felix Tshisekedi na rais wa tume ya AU Moussa Faki wameitisha mkutano wa dharura wa taasisi za umoja huo kuhusu usalama na Amani ili kutathmini hali nchini Guinea na kuchukua hatua zifaazo
hapo jana katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres ametuma ujumbe wa twitter akijibu kinachotokea Guinea.Amesema kwamba anafuatilia hali hiyo kwa karibu.
Aliongeza kuwa alilaani kuchukuliwa kwa serikali kwa nguvu ya bunduki na akataka kuachiliwa mara moja kwa Rais Alpha Conde.
Hatima ya Rais wa Guinea Alpha Condé haijulikani wazi baada ya video ambayo haijathibitishwa kumuonyesha mikononi mwa wanajeshi, ambao walisema wamefanya mapinduzi.
Walakini, waziri wa ulinzi amenukuliwa akisema jaribio la kuichukua serikali lilikuwa limeshindwa.
Hii inafuatia masaa mengi ya makabiliano ya risasi karibu na ikulu ya rais katika mji mkuu, Conakry.
Jeshi ambalo limedai kuchukua madaraka nchini humo limetangaza kwamba litafanya mkutano leo na mawaziri na wakuu wa taasisi zilizovunjwa jana mjini Conakry.Wanajeshi hao pia wametangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku .
Bado haijulikani ni nini kinatokea huko Conakry, lakini wanajeshi wanasema wamechukua udhibiti. Katika hotuba iliyoonyeshwa kwa njia ya televisheni, wanaume walio na sare za kijeshi, bendera ya Guinea ikiwa nyuma yao wamelihutubia taifa
Wakijiita Kamati ya Kitaifa ya upatanisho na maendeleo, wanalaumu ufisadi uliokithiri, usimamizi mbaya na umasikini nchini Guinea kwa uamuzi wao wa kufanya mapinduzi. Wanasema katiba imevunjwa na kwamba kutakuwa na mashauriano ya kuunda mpya, inayowahusisha watu wote .
Chanzo cha picha, AFP
Wamedai pia kwamba serikali imevunjwa na kwamba mipaka ya ardhi itafungwa kwa wiki moja.
Katika picha na video zilizowekwa katika mitandao ya kijamii, mtu ambaye anaonekana kuwa rais Alpha Condé, amevaa mavazi ya kawaida na shati iliyochapishwa maua anaonyeshwa akiwa amekasirika akiwa amezungukwa na wanaume walio na sare za jeshi.
Katika video moja, ameulizwa kwa Kifaransa ikiwa ameumizwa kwa njia yoyote lakini hajibu.
Ubalozi wa Australia umewauliza raia wake kukaa mahali salama na kutazama vyombo vya habari vya ndani na taarifa kutoka kwa balozi.
Kumekuwa na ripoti nyingi za milio ya risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi Jumapili asubuhi.
Wakazi wa eneo hilo wameambia mashirika ya habari kuwa wanajeshi wamekuwa wakifanya doria mitaani na wamefunga daraja kuelekea mtaa ambao ikulu ya rais iko.
Wakazi wenye hofu ya wilaya kuu ya Kaloum wametii maagizo yao ya kukaa nyumbani.
Daraja la pekee linalounganisha bara na eneo la Kaloum, ambalo lina wizara nyingi na ikulu ya rais, lilikuwa limefungwa na wanajeshi wengi, wengine wakiwa na silaha nzito, walikuwa wamewekwa kuzunguka ikulu, chanzo cha jeshi kiliambia Reuters.
Video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha misafara ya magari ya kubeba silaha na malori yanayobeba askari wanaofanya doria mitaani, ingawa hizi hazijathibitishwa.
Mechi ya kombe la dunia yaahirishwa
Kufuatia machafuko nchini Guinea ,mchuano wa timu ya taifa hilo wa kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Morocco nyumbani uliofaa kuchezwa leo umeahirishwa .
Shirikisho la soka duniani Fifa limesema uamuzi huo ulichukuliwa ili kulinda usalama wa wachezaji na maafisa wa mechi .
Timu ya Morocco imenaswa nchini hmo baada ya mapinuzi hayo na inaripotiwa kungoja kupata idhini ya ubalozi kusafiri hadi uwanja wa ndege .
Rais Conde alichaguliwa kwa muhula wa tatu uliokumba na utata ambao ulisababisha ghasia mwaka jana .Mwanasiasa huyo mkongwe alichaguliwa mara ya kwanza kuwa rais mwaka wa 2010 katika uchaguzi wa kwanza ulioshuhudia makabidhiano ya mamlaka ya njia ya Amani .
Licha ya utawala wake kufanikiwa kuboresha hali ya uchumi amelaumiwa kwa kuongoza serikali inayokiuka haki za binadamu na unyanyasaji wa wakosoaji wake .