Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kumalizia kifungo chake nyumbani kwasababu za kitabibu

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amepewa msamaha wa matibabu. Idara ya huduma za marekebisho nchini humo ilitoa taarifa muda mfupi uliopita ikithibitisha kuwa rais huyo wa zamani atamalizia kifungo chake nyumbani.

Idara ya huduma za marekebisho nchini Afrika Kusini imesema Rais wa zamani Jacob Zuma yuko hospitalini akipata matibabu ya maradhi ambayo hayajafahamika.

Idara hiyo ilisema rais huyo wa zamani anayetumikia kifungo jela alifanyiwa upasuaji mwezi uliopita na kwamba hawawezi kufichua kile anachosumbuliwa nacho lakini anaweza tu kuthibitisha kuwa walipokea ripoti zaidi ya moja ya matibabu.

Bwana Zuma sasa amewekwa kwenye msamaha wa matibabu kwa sababu ya afya yake.

Hii inakuja karibu miezi miwili baada ya rais wa zamani kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau na Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini.

Bwana Zuma atatumikia kifungo kilichobaki nyumbani na wakfu wake umekaribisha hatua hiyo.

Wanajeshi waliingia mtaani kudhibiti vurugu siku chache baada ya kukamatwa kwa rais huyo wa zamani kutokana na maandamano ya vurugu na uporaji uliotokea katika mkoa wa nyumbani kwake wa Kwa-Zulu na Gauteng, kitovu cha uchumi cha Afrika Kusini.

Wakati huo huo Bwana Zuma anatarajiwa kufika mahakamani Jumatano kwa kuendelea kwa kesi yake ya ufisadi ambapo anatuhumiwa kupokea rushwa inayohusiana na mpango wa silaha ambao ulifanyika mnamo miaka ya 1990