Khalid Sheikh Mohammed: Jinsi aliyepanga 'shambulizi la 9/11' alivyoponyoka mikononi mwa FBI

Courtroom sketch

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mohammed akiwa mahakamani mwaka 2012

Mtu anayetuhumiwa kwa kupanga njama mbaya ya uvamizi wa ndege za abiria zilizotekwa nyara Marekani miaka 20 iliyopita amezuiliwa gerezani akisubiri kesi.

Lakini je, pengine angeweza kuzuiwa miaka iliyotangulia?

"Alikuwa kijana wangu."

Frank Pellegrino alikuwa amekaa katika chumba cha hoteli huko Malaysia wakati alipoona picha kwenye televisheni za ndege zikianguka kwenye Jumba la Twin Towers.

Jambo la kwanza alifikiria lilikuwa: "Mungu wangu, lazima awe ni Khalid Sheikh Mohammed."

Lengo na matamanio yalikuwa sawa na Pellegrino sasa alikuwa katika nafasi ya kipekee kujua ukweli.

Aliyekuwa jasusi maalum wa FBI alikuwa amemfuatilia Mohammed kwa karibu miongo mitatu, lakini yule anayedaiwa kuwa mtekelezaji wa mashambulizi ya 9/11 bado hajakabiliwa na haki.

Wakili wa Mohammed ameiambia BBC, inaweza kuchukuwa miaka mingine 20 kabla ya kesi hiyo kuhitimishwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Bush anajumuika na zimamoto kuondoa vifusi siku kadhaa baada ya shambulizi

Osama Bin Laden, wakati huo akiwa kiongozi wa kundi la al-Qaeda, ndiye mtu anayehusishwa kwa karibu na mashambulizi ya 9/11. Lakini uhalisia ni kwamba Mohammed - au "KSM" kama alivyokuwa akifahamika - ndiye aliyekuwa "mratibu mkuu", kulingana na Tume ya Uchunguzi ya 9/11 iliyochunguza mashambulizi hayo. Ndiye mtu aliyekuja na wazo hilo na kulipeleka kwa al-Qaeda.

Akiwa mzaliwa wa Kuwait, alisomea Marekani kabla ya kupigana nchini Afghanistan katika miaka ya 1980.

Miaka kadhaa kabla ya shambulio la 9/11, jasusi wa FBI Frank Pellegrino alikuwa kwenye kesi ya jihadi.

Pellegrino alikuwa amepewa jukumu na FBI kuchunguza shambulizi la bomu la mwaka 1993 la Kituo cha Biashara Ulimwenguni.

Hapo ndipo jina la Mohammed lilipoanza kuvutia nadhari katika maamlaka ya Marekani kwa mara ya kwanza kwasababu alikuwa amehamisha pesa kwa mmoja wa wale waliohusika.

Jasusi huyo wa FBI alitambua ukubwa wa azma ya Mohammed mnamo mwaka 1995 wakati alihusishwa na njama ya kulipua ndege nyingi za kimataifa juu ya Pasifiki.

Katikati ya miaka ya 1990, Pellegrino alikuwa karibu kumnasa mtu wake, akimfuatilia hadi Qatar.

Yeye na timu yake walikwenda Oman ambapo walipanga kuvuka kuingia Qatar na kumkamata Mohammed.

Ndege ilikuwa tayari kumsafirisha mtuhumiwa.

Lakini kulikuwa na upinzani kutoka kwa wanadiplomasia wa Marekani juu waliokuwepo wakati huo.

Pellegrino alikwenda Qatar na kuambia balozi na maafisa wengine katika ubalozi kwamba alikuwa na mashtaka dhidi ya Mohammed ya njama hiyo inayohusu ndege.

Lakini anasema walionekana kuwa na wasiwasi wa kusababisha matatizo kwa nchi hiyo.

"Nadhani walifkiri kwamba hii itasababisha matatizo ," Pellegrino anakumbuka.

Chanzo cha picha, Frank Pellegrino

Maelezo ya picha,

Pellegrino mwaka 1987 na mwaka 2020

Hatimaye balozi alimjulisha Pellegrino kwamba maafisa wa Qatar wamedai kumpoteza Mohammed kwa maana ya alipo.

"Kulikuwa na hofu, hasira na kuchanganyikiwa," anasema.

"Tulijua wakati huo ilikuwa ni nafasi iliyopotea"

Lakini anakubali kuwa katikati ya miaka ya 90, Mohammed hakuonekana kama mlengwa anayestahili kupewa kipaumbele.

Pellegrino hakuweza hata kumfanya aorodheshwe kwenye orodha ya watu 10 wanaosakwa mno na Marekani.

"Niliambiwa kwamba tayari kuna magaidi wengi huko."

Mohammed anaonekana kuarifiwa juu ya lengo la Marekani kwake na kukimbia Qatar, ambako aliishia nchini Afghanistan.

Kwa miaka michache iliyofuata, jina la KSM liliendelea kujitokeza, mara nyingi katika orodha ya simu ya washukiwa wa ugaidi waliokamatwa kote ulimwenguni, na kuweka wazi kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu nao.

Ilikuwa katika miaka hii alipoenda kwa Bin Laden na wazo la kufundisha marubani kuendesha ndege ndani ya majengo Marekani.

Na kisha shambulizi la 9/11 likatokea.

Mashaka ya Pellegrino juu ya jukumu la KSM yakathibitishwa kuwa kweli wakati mtu muhimu wa al-Qaeda aliyekuwa kizuizini alipomtambua.

"Kila mtu alitambua kwamba aliyekuwa akitafutwa na Frank ndiye aliyeratibu kitendo hicho," Pellegrino anakumbuka.

"Tulipogundua kuwa alikuwa yeye, hakukuwa na mtu aliyeonekana mnyonge zaidi yangu."

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Shambulio la bomu katika Kituo cha Biashara Duniani mwaka 1993 lilisababisha vifo vya watu 6 huku wengine zaidi ya 1,000 wakijeruhiwa

Mnamo mwaka 2003, Mohammed alifuatiliwa na kukamatwa nchini Pakistan.

Pellegrino alitumai atashtakiwa chini ya mashtaka ambayo alikuwa ameyafanyia kazi.

Lakini akatoweka.

Shirika la kijasusi la Marekani (CIA) lilikuwa limempeleka kwenye "eneo maalum" kutumia "mbinu mbalimbali za kisasa kumuhoji."

"Nataka kujua anayojua, na nataka kujua kwa haraka sana" afisa mwandamizi wa CIA alisema wakati huo.

Mohammed aliteswa kwa kutiwa ndani ya maji angalau mara 183, kitu kilichoelezewa kama "kuwa karibu kufa maji". Alipata lishe yake kwa njia ya kuwekwa mpira katika njia ya haja kubwa, msongo wa mawazo, kukosa usingizi, kuwa uchi kwa kulazimishwa, na aliambiwa watoto wake watauawa.

Alikiri kutekeleza njama nyingi wakati huo.

Lakini ripoti ya Seneti baadaye iligundua kuwa taarifa nyingi zilizotolewa zilikuwa zimebuniwa tu na mfungwa huyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Taarifa kutoka kwa Mohammed zilipelekea utafutaji wa kina wa Osama Bin Laden katika mpaka wa Pakistani

Baada ya maelezo ya mpango wa CIA kutolewa, " wafungwa waliokuwa wanatakiwa sana" kama Mohammed walihamishiwa gereza la Guantanamo Bay mnamo mwaka 2006. Hatimaye shirika la FBI likaruhusiwa kuendeleza uchunguzi wake.

Mnamo Januari 2007 Frank Pellegrino alikutana uso kwa uso na mtu aliyemfuatilia kwa muda mrefu.

Wanaume hao walikaa karibu katika meza wakiangaliana.

"Nilitaka kumjulisha nimehusika katika kumshtaki yeye miaka ya 90," anasema, kwa matumaini ya kuanzisha mazungumzo ili kupata habari kuhusu shambulizi la 9/11.

Afisa huyo wa zamani wa FBI hakutoa maelezo ya kile walichozungumza lakini alikubali kuwa "yeye ni mtu mcheshi, amini usiamini".

Mara nyingi KSM ameonekana kuwa "vizuri" wakati wa kusikilizwa kwa kesi huko Guantanamo na Pellegrino anamuelezea mshukiwa huyo maarufu wa ugaidi ulimwenguni kama "Kardashian" katika kutamani kuangaziwa lakini anasema haonyeshi kujutia matendo yake.

Je! Angekiri au angependa kutumia vyema kesi hiyo?

"Kwa kweli nadhani kwake anaona ni sawa na yale aliyoyafanya, lakini anapenda sana kipindi hicho," anasema.

Baada ya kuzungumza na Mohammed kwa siku sita, hatimaye alisema alikuwa amepitia ya kutosha.

"Na hivyo ndivyo ilivyokuwa," anakumbuka Pellegrino.

Majaribio ya baadaye ya kupatikana kwa haki kutokana na shambulio la 9/11 yamepungua.

Mpango wa kufanya kesi huko New York uliyumba baada ya kupata upinzani kutoka kwa umma na kisiasa.

"Kila mtu alikuwa akipiga kelele", Sitaki kumuona mtu huyu nyuma ya uwanja wangu. Mumuweke huko Guantanamo, " anasema Pellegrino, yeye mwenyewe akiwa ni raia wa New York.

Maelezo ya video,

Ndani ya gereza la Guantanamo Bay

Kilichofuata ilikuwa ni mahakama ya kijeshi huko Guantanamo.

Lakini mchakato wa kiutaratibu ukachelewa, uliojumuishwa na janga la Covid-19 na kusababisha kufungwa kwa gereza hilo, pia kumechangia mchakato huo kuendelea kwa muda mrefu.

Kesi hiyo itasikilizwa sana wiki hii lakini mwisho wake unaonekana kuwa mbali sana.

Wakili wa Mohammed anaamini vikao vya kusikilizwa kwa kesi vya hivi karibuni vimepangwa kuonyesha vyombo vya habari kuwa kuna jambo linafanyika kwenye kumbukumbu ya miaka 20 ya shambulizi la 9/11.

David Nevin aliiambia BBC kuwa "anatarajia maendeleo fulani ili kukamilika kwa mchakato huo"

Wakili anayemtetea mshukiwa, amekuwa kwenye kesi hiyo tangu ilipoanza mnamo mwaka 2008. Mpango wa asili ulikuwa kuanza kusikilizwa kwa kesi mara moja. Lakini bado hawajakaribia hata kuanza kusikilizwa kwa kesi, anasema, jaji mpya aliyeteuliwa ni "jaji wa nane au wa tisa ambaye tumekuwa naye," kulingana na jinsi unavyohesabu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Picha ya mtu anayetafutwa na Marekani ikitolewa na Rais Bush mwaka 2001

Jaji anapaswa kujifahamisha na kesi hiyo yenye kurasa 35,000 za nakala za vikao vya awali na maelfu ya hoja katika kile Nevin anafafanua kama "kesi kubwa za jinai katika historia ya Marekani"

Na ndio yenye utata zaidi.

Hiyo ni kwasababu washtakiwa watano wote walishikiliwa kizuizini kwa siri na CIA na kufanyiwa "mbinu za kisasa za kuhojiwa".

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Eneo la Guantanamo ambapo baadhi ya kesi zimesikilizwa awali

Hata hivyo, hatua hiyo imesababisha hoja juu ya ushahidi kuchafuliwa na kile kilichotokea katika maeneo ya siri waliozuiliwa.

Marekani "iliandaa na kutekeleza mpango uliofafanuliwa wazi kuwatesa wanaume hawa," anasema Nevin.

Njia hizo hutoa wigo mpana wa rufaa dhidi ya hukumu yoyote inayoendelea kwa miaka.