Samia Suluhu: Tanzania kuhudhuria Kikao cha Umoja wa Mataifa kuna tafsiri gani?

  • Mohammed AbdulRahman
  • Mchambuzi
Ukumbi wa mikutano ya Umoja wa Mataifa mjini New York
Maelezo ya picha,

Ukumbi wa mikutano ya Umoja wa Mataifa mjini New York

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan yuko mjini New York, kuhudhuria Kikao cha wiki moja cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kilichoanza Jumanne.

Uamuzi huo unaangaliwa kuwa ni mabadiliko ya muelekeo katika sera ya mambo ya nchi za nje ikilinganishwa na miaka takriban 6 iliyopita ya uongozi wa mtangulizi wake, Rais John Magufuli aliyefariki Dunia Machi 2021. Je safari yake ina malengo gani?

Rais Magufuli hakufanya hata ziara moja nje ya Bara la Afrika na alikuwa akisisitiza kwamba yeye kwake kipaumbele kilikuwa kushughulikia maendeleo ya taifa hilo. Alijikita zaidi katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu. Kwa kiasi kikubwa msimamo huo ulizorotesha zaidi nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Taifa hilo la Afrika mashariki lilikuwa sawa na msemaji wa Afrika katika masuala ya Kimataifa katika majukwaa kama Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote, Jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo Kusini mwa Africa SADC na katika Umoja wa Mataifa.

Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wake wa kwanza, Mwalimu Juliua Nyerere iliongoza pia kampeni ya kuunga mkono harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kupitia lile kundi lililojulikana kama mataifa ya mstari wa mbele. Mataifa hayo yalikuwa Tanzania, Zambia, Botswana, Msumbiji na Angola.

Katika Umoja wa Mataifa aliyekuwa mwakilishi wake wa kudumu, Dr Salim Ahmed Salim, aliiongoza Kamati ya Umoja huo ya Kupambana na Ukoloni (UN Decolonization Committee), kwa kipindi cha miaka 10 akiwa Mwenyekiti wa kamati hiyo. Tanzania ilikuwa "akisema anasikika."

Tangu alipofariki Mwalimu Nyerere October1999 baada ya kustaafu na kukabidhi uongozi kwa mrithi wake, Ali Hassan Mwinyi, sauti na haiba ya Tanzania katika siasa za Afrika na dunia ilianza ilianza kupungua taratibu, licha ya kwamba iliendelea kwa kiasi fulani wakati utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete.

Taswira ya ushirikiano wa kimataifa

Rais Samia Suluhu ameingia madarakani kumrithi Magufuli akiwa na mtazamo tofauti na mtangulizi wake. Anaonekana ameazimia kuirejesha tena Tanzania katika kundi la nchi zenye ushawishi barani Afrika. Akiwa amejikita zaidi katika kuwavutia wawekezaji na kufungua nafasi kwa vitega uchumi, ili kuimarisha uchumi wa taifa hilo, ameuona umuhimu wa kujongeleana na nchi nyingine.

Njia mojawapo ni kushiriki mikutano ya taasisi mbali mbali na kupata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi na watendaji kutoka nchi nyingine, ili kujenga ushirikiano na mazingira ya kuaminiana. Rais wa zamani Jakaya Kikwete aliamini ziara za nje kutafuta uwekezaji na kupata masoko ya biashara ni muhimu kwa uchumi.

Serikali yake ikafunga mikataba kadhaa na wawekezaji ikiwa ni pamoja na katika sekta ya madini. Wakati fulani Kikwete aliwahi kutamka "Usipokuwa tayari kuliwa kidogo, huli" aliposhika madaraka Magufuli aliikosoa na hata kuifuta baadhi ya mikataba.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Uamuzi wa Rais Samia Suluhu kushiriki binafsi katika kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu ni sehemu ya mkakati wa mabadiliko. Nafasi ya kukutana ana kwa ana na viongozi wengine ni njia ya kujenga ushirikiano wa nchi zao. Tanzania inaazimia kufikia daraja ya uchumi wa kati na ushirikiano imara na wa kuaminika na nchi nyingine ni muhimu katika kufikia daraja hiyo.

Tayari ameanza kile kinachoitwa diplomasia ya kiuchumi na kuzizuru nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda ambazo sawa na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau muhimu katika uchumi na biashara na mataifa ya kigeni, kinyume na kipindi cha Rais Magufuli ambapo uhusiano na nchi jirani hususan Kenya ulizorota.

Akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Aprili 2021 baada ya kushika hatamu za Urais Machi 19, Rais Samia Suluhu alisisitiza juu ya mkakati wa serikali yake wenye lengo la kuongeza uchumi, akikiri kwamba mazingira yaliokuwepo hayakuwa muafaka kwa wawekezaji na kuahidi mabadiliko ya sheria zinazohusika na uwekezaji ili kuwavutia zaidi wawekezaji.

Vile vile akazungumzia umuhimu wa kupunguza urasimu na kupambana rushwa, ili kuleta ufanisi. Maendeleo ya kiuchumi hayawezi kustawi bila kuwa na utulivu na usalama. Kuwepo kwa Rais Samia Suluhu katika hadhara hiyo Kuu ya Umoja wa Mataifa pia kuna umuhimu wake katika suala la usalama na vita dhidi ya ugaidi.

Vita dhidi ya Ugaidi

Nchi kadhaa barani Afrika zinakabiliwa na kitisho cha usalama kutokana na harakati za kigaidi za makundi ya itikadi kali za kidini baadhi yakidai kuwa na uhusiano na Al-Qaeda au Dola la Kiislamu-ISIS. Mtihani mkubwa unaendelea kuzikabili nchi za ukanda wa Sahel na Afrika magharibi kuanzia Mali, Niger, Burkina Faso hadi Nigeria.

Zote zimekumbwa na mashambulio ya mara kwa mara na mauaji na kitisho hicho kimesogea pia kusini mashariki mwa Afrika nchini Msumbiji. Tangu 2017 Msumbiji imekumbwa na mashambulio ya wanamgambo wa Kiislamu katika mkoa wake wa Cabo Delgado wanaojulikana kama Al-Shabab.

Wanamgambo hao wanadai hawana mafungamano yoyote na kundi la Al-Shabab la Somalia, ambalo mnamo miaka ya nyuma limekuwa kitisho kikubwa kwa Kenya. Kenya iliyoshuhudia mashambulio ya kundi hilo mara kadhaa inaendelea kuchukua hatua za tahadhari, licha ya kwamba harakati za Al-Shabab kwa kiasi fulani zinaonekana kupungua.

Mkoa wa Msumbiji wa Cabo Delgado unapakana na Tanzania na harakati za kundi hilo la itikadi kali zimeitia hofu nchi hiyo jirani na kusababisha kuimarisha shughuli zake za ulinzi na usalama katika maeneo ya mpakani hususan mkoa wa Mtwara.

Aprili mwaka huu, Rais Samia Hassan alihudhuria mkutano wa dharura wa Viongozi Wakuu wa nchi na Serikali wa Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC mjini Maputo, Msumbiji ambapo miongoni mwa masuala makuu lilikuwa lile la kupambana na ugaidi.

Bila shaka suala la ugaidi likiwa ni la dunia kwa jumla bado ni huenda likawa sehemu ya majadiliano mjini New York, iwe ni katika ajenda au pembezoni mwa kikao hicho. Kwa mujibu wa ratiba Rais Samia Suluhu amepangiwa kulihutubia Baraza Kuu siku ya Alhamisi Septemba 23.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Wajumbe katika baraza la umoja wa mataifa mjini New York

Tutarajie nini katika hotuba ya Rais Samia Alhamisi?

Inatarajiwa huenda miongoni mwa mambo mengine akagusia juu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa Tanzania, na athari za janga la UVIKO-19 (Covid-19) pamoja na siasa za kanda na kimataifa, huku wadadisi wakijiuliza kama atagusia juu ya hali ya kisiasa ndani ya Tanzania.

Utawala wake unakosolewa na wapinzani na wanaharakati wanaopigania demokrasia ndani na nje, kwa kuendeleza kile wanachodai ni hatua zile zile za kukandamiza demokrasia na uhuru wa kukusanyika zilizochukuliwa na mtangulizi wake John Magufuli. Rais Samia Suluhu aliahidi hapo awali kubadili mkondo huo, ahadi iliyotoa matumaini ambayo sasa yanafifia.

Kwa wakati huu mvutano kati ya upinzani umezidi kutokana na kuanza kupazwa sauti za kudai Katiba mpya, jambo ambalo Rais huyo amesema linaweza kusubiri kwanza. Pia kukamatwa na kushtakiwa kwa kiongozi wa chama mashuhuri cha upinzani CHADEMA, Freeman Mbowe na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi, kumeibua hali ya sintofahamu na serikali.

Kwa zingatio la yote kwa jumla, hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan mbele ya Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inasubiriwa kwa hamu kubwa.

Kwa upande wa viongozi wengine wa Afrika, mbali na masuala mengine kama njaa na migogoro kipaumbele kwao ni suala kuu ambalo ni kukabiliana na janga la Covid-19 na athari zake.