Waridi wa BBC: Niliolewa nikiwa na umri wa miaka 13 na mtu nisiyemjua

  • Anne Ngugi
  • BBC Swahili
Niliolewa nikiwa na umri wa miaka 13 na mtu nisiyemjua

Chanzo cha picha, Asha Ake

Maelezo ya picha,

Niliolewa nikiwa na umri wa miaka 13 na mtu nisiyemjua

Aisha Ake ni mwanamke mwenye umri wa miaka 26 aliyeingia katika maisha ya ndoa tangu akiwa na umri wa miaka 13.

Kwake yeye kipindi chote cha ndoa yake amekuwa akikiona kama ndoto kwasababu hakufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Yeye ni miongoni mwa wasichana ambao wanatoka katika jamii zinazoruhusu ndoa za mapema miongoni mwa wasichana wadogo.Ndoa za utotoni ni kinyume cha sheria nchini Kenya .

"Niliozwa. nikiwa mtoto hata sikuwa nafahamu mume hufanyiwa wala kujua majukumu ya ndoa , kwa kweli nilikuwa mtoto machoni mwa mume wangu "anakumbuka Aisha

Alivyofungishwa ndoa akiwa msichana mdogo

Aisha ambaye ni mzaliwa wa eneo la Moyale , Kaskazini mashariki mwa Kenya , anasema kuwa alilelewa na mama wa kambo ,tangu alipokuwa na umri mdogo wa miaka 2 .

'Nilipofika darasa la tano nikielekea la sita hapo, ndipo nilianza kupata fahamu kuhusu hayo yote. Ni wakati huohuo nilipogundua kwamba sina uhusiano mzuri na mama wa kambo, hivyobasi nikawa sina uhuru uwezo wa kuzungumza naye wazi kuhusu mambo yaliokuwa yananisumbua kama binti,"anakumbuka Aisha

Mwanadada huyu anasema ni wakati huo ambapo mama wa kambo alimuita na kumueleza kuwa kulikuwa na mwanamume mmoja aliyekuwa na lengo la kumuoa .

"Unakumbuka wale watu walikuja kututembelea , na yule kijana walikuwa naye , wamesema wanataka kukuoa '', ni matamshi yaliotoka katika kinywa cha mamake wa kambo .

''Nilishtuka sana nisijue cha kufanya , na kwasababu sikuwa na uwezo wa kukataa au kuuliza chochote nilinyamaza kimya huku moyo ukinidunda kwa kasi"

Ilikuwa kati ya mwaka 2006 na 2007, na tangu wakati huo maisha yake yalichukua mkondo tofauti na ukawa mwanzo wa mchakato wa maisha mapya ya ndoa akiwa na umri wa miaka 13.

Chanzo cha picha, Asha Ake

Maelezo ya picha,

Alilazimika kusafiri hadi Moyale, licha ya kuelezewa kwamba babake mzazi alipinga kufanyika kwa ndoa hiyo akiwa na umri mdogo.

Wakati huo wote Aisha anasema baba yake alikuwa katika mji mkuu,Nairobi.

Alilazimika kusafiri hadi Moyale, licha ya kuelezewa kwamba babake mzazi alipinga kufanyika kwa ndoa hiyo akiwa na umri mdogo.

Hatahivyo mama ya mume wake alitoa hakikisho kwa baba na mama kuwa atahakikisha amekamilisha shule na kuishi maisha mazuri .

Kutokana na heshima iliyokuwa kati ya jamii hizo mbili hivyo ndivyo Aisha alivyofungishwa ndoa rasmi.

Cha ajabu ni kuwa mwanadada huyo hakumfahamu mtu aliyekuwa awe mume wake, kwasababu katika jamii yao lilikuwa jambo la kawaida kwa binti kuozwa bila hata kufahamu mume wake.

Mchakato wa kufunga ndoa

'Siku moja mwaka wa 2006 nilikuwa najiandaa kumaliza darasa la saba ili hatimaye nijiunge na darasa la nane kwa lengo la kukamilisha masomo yangu ya msingi''.

Ilikuwa wiki moja kabla ya kufanyika kwa harusi ,ambapo msichana huyo alipelekwa sehemu moja ambayo kulingana na jamii yao wasichana wanaotarajiwa kuolewa hupelekwa ili wafanyiwe mapambo na mila nyengine.

Lakini kwa Aisha haya yote yalikuwa mageni kwake.

Kwa kuwa ni mila na desturi kwa bibi harusi kusalia nyumbani siku chache kabla ya harusi , mwanadada huyo anasema kipindi chote hicho alifungiwa asiwe na uwezo wa kutoka nje.

Chanzo cha picha, Asha Ake

Maelezo ya picha,

Kwa kuwa ni mila na desturi kwa bibi harusi kusalia nyumbani siku chache kabla ya harusi , mwanadada huyo anasema kipindi chote hicho alifungiwa asiwe na uwezo wa kutoka nje.

Hakuweza kuwaona marafiki zake , na waliofaulu kumuona walikuwa wanamsalimia kupitia dirishani pekee.

Anasema kwamba hilo lilifanywa kwa lengo la kumzuia mtu yeyote kumshawishi kukataa kuolewa wakati huo .

Mwanadada huyo anasema kuwa wiki hio ilikuwa ya majonzi.

Anasema kwamba baada ya siku saba walifunga ndoa na baadaye akasafirishwa hadi mji wa Marsabit yapata kilomita kadhaa kutoka mji wa Moyale alipokuwa akiishi kabla ya ndoa yake.

''Niliozwa nikiwa na umri wa miaka 13 na mume wangu pia alikuwa na umri mdogo kwasababu naye alikuwa amekamilisha kidato cha nne - na kwamba mimi nilikuwa kama zawadi yake kwa kumaliza Shule''..

"Niliozwa Nikiwa na umri miaka 13 nilikuwa mtoto mdogo bado , hata huyo mume naye alikuwa sio mkubwa, alikuwa ndio amekamilisha kidato cha nne , mimi nilikuwa kama zawadi'', alisema.

Chanzo cha picha, Asha Ake

Maelezo ya picha,

''Niliozwa nikiwa na umri wa miaka 13 na mume wangu pia alikuwa na umri mdogo kwasababu naye alikuwa amekamilisha kidato cha nne - na kwamba mimi nilikuwa kama zawadi yake kwa kumaliza Shule''..

Kulingana na Aisha, mume wake alifunga ndoa naye kabla ya kupata matokeo ya kidato cha nne .

Usiku wa kwanza ndani ya ndoa

Kwasababu hawakuwa wanafahamiana na mume wake ilikuwa vigumu wao kujamiana usiku wake wa harusi..

"Nilifika sehemu ambayo sikujua chochote , na sikumfahamu yoyote , nilikuwa tu nalia kila wakati , hata nikihisi njaa au kwenda haja zangu sikuwa ninasema nilikuwa muoga sana'

Aisha anasema kuwa hakuamini alikuwa ni mke wa mtu , na kuongezea kuwa alihisi ameondoka katika familia yake ili kulelewa na familia tofauti kwasababu kila kitu kilikuwa kikifanywa na mamake mume wake kuanzia kupika , usafi na kadhalika .

"Mimi hata sikuwa najua kupika , pengine chai na kahawa peke yake , tulikuwa tunaishi na baba na mama mkwe , sikuwahi kujichukulia kama mke wa mtu na kwamba nilikuwa na nyumba yangu kwasababu mama mkwe ndiye aliyekuwa akishughulika na kila kitu nyumbani", aliongezea Aisha.

Baada ya miezi michache akiwa katika ndoa, binti huyo alipata ujauzito . Na ilipofika wakati wa kujifungua, Aisha hakuweza kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyobasi akalazmika afanyiwe upasuaji.

Akiwa katika harakati hizo za upasuaji alipoteza fahamu kwa siku 10. Cha kuhuzunisha ni kuwa alimpoteza mtoto huyo kwani kulingana na wakunga alifariki masaa machache tu baada ya kuzaliwa .

"Nilipoamka niliwakuta watu wamenizunguka , nilishtuka na kuwauliza mtoto wangu yuko wapi , walinieleza aliaga , nililia kwa uchungu mwingi nisijue cha kufanya'' , alielezea msichana huyo.

Baada ya siku kadhaa Aisha alirejeshwa nyumbani ili kuuguza jeraha la upasuaji.

Hatahivyo maisha yalianza kubadilika baada ya miaka mitatu ya ndoa .

Ni masaibu ambayo yalimkuta binti huyo kwa muda mrefu na hakuwa na wa kumwambia.

Mwaka 2009 alipata ujauzito mwengine na akajifungua mtoto.

Kipindi chote cha ndoa hakuhisi kwamba alikuwa mke wa mtu kwasababu majukumu mengi ya nyumbani yalikuwa kati ya baba na mama mkwe.

Chanzo cha picha, Asha Ake

Maelezo ya picha,

Asha anasema kuwa mume wake alijiunga na chuo kikuu na akaanza kuwa na mienendo tofauti isio ya kawaida

Wakiwa katika ndoa yao walitofautiana kila mara na mume wake kwasababu wote walikuwa na fikra zilizokosa a ukomavu na hata alipokuwa akipitia usumbufu wa nyakati za asubuhi akiwa mja mzito hakufahamu kwamba alikuwa na ujauzito .

Baada ya miezi minane alipata ujauzito mwengine ambao ulimletea misukosuko.