Kabiru Alhassan: 'Mke wangu alikataa kuolewa na mtu mwenye mikono miwili’

Kabiru with an ax

Mtema kuni Kabiru Alhassan ameendelea kuzua gumzo nchini Nigeria baada ya Idhaa ya BBC Pidgin kuangazia simulizi yake katika video akielezea jinsi mke alivyokataa kuolewa na mtu aliye na mikono miwili.

Kabiru mwenye umri wa miaka 38, mkaazi wa Kano kaskazini magharibi mwa Nigeria anasema ameishi na mke wake kwa miaka 13 na hajawahi kumdunisha kwa sababu ana mkono mmoja.

"Huwezi kuamini aliachana na mchumba ambaye tayari alikuwa amemtambulisha kwa wazazi wake na kunifuata mimi nilipomwambia nampenda."

"Kutokea wakati huo hadi wa leo safari yetu ya ndoa imekuwa ya furaha. Hajawahi kunifanyia kitu ambacho kinanikumbusha kuwa sina mkono mmoja. Namshukuru sana kwa hilo.

Kabiru alipoteza mkono wake mmoja miaka 22 iliyopita baada ya kuanguka kutoka juu ya mti na kuvunjika alikuwa kijijini kwao nje kidogo ya. Familia yake ilimpeleka kwa tabibu wa kienyeji.

"Wiki chache baada ya tabibu kuunganisha mkono wangu ulianza kuoza, ndipo nikakimbizwa hospitali ambapo daktari alisema jinsi ulivyo sina budi kuupoteza wangu."

Kabiru anasema kuwa anapata hadi N1500 au N2000 kutokana na uuzaji kuni.

"Biashara ya kuuza kuni ni biashara kama nyingine yoyot, kuna siku ni nzuri na kuna siku ambazo biashara sio nzuri.

"Kuna siku wateja wanakupigia simu uwavunjie kuni nyingi siku kama hizo unaweza kupata hadi N2000

"Na siku nyingine unatoka sokoni bila senti mfukoni."

Sani Munjibir ambaye pia ni mtema kuni mwenzake amemjua Kabiru kwa zaidi ya miaka 10 na anapenda kumuita KB akisema anafanya kazi yake kwa bidii lich aya kuwa na mkono mmoja.

"Mara ya kwanza tulishangaa jinsi navyofanya kazi lakini baadaye tulizoea, anafanya kazi zaidi hata zaidi ya watu waliyo na mikono miwili."

"Anaweza kupasua kuni ngumu ambazo zinatumiwa kuoka mikate, kwa hivyo nashukuru sana."

Kingine anachojivunia mtema kuni huyu ni kwamba hatumii kinywaji chochote cha kuongeza nguvu.

''Situmii kitu chochote cha kuongeza nguvu, huu ni uwezo tu kutoka kwa Mungu. Baada ya shughuli za siku naenda nyumbani kuoga, kumpumzika na kuendelea na kazi siku inayofuata.

Kabiru aliambia BBC Pidgin kuwa anamtunza mama yake mzee na familia yake, akiongeza kuwa angelifurahia sana laiti angelipata mtaji wa kuanzisha biashara nyingine kwani mkono wake huo mmoja umechoka kutokana na kazi ngumu anazofanya.

Kwa sasa hana budi kuendelea na ukataji kuni.