India: Polisi 'watibua jaribio la mtu kughushi kifo chake '

Prisoners hands emerging from a jail cell

Chanzo cha picha, Getty Images

Polisi wa India wanasema wamezuia njama ya mtu aliyejaribu kughushi kifo chake ili kuepuka kurejeshwa gerezani.

Maafisa katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh wanasema Sudesh Kumar, 36, alimuua mwanaume mmoja na kujaribu kuupitisha mwili huo kama wake kwa msaada wa mke wake.

Lakini polisi walipata picha za CCTV akiubeba mwili huo kwenye baiskeli.

Kumar aliripotiwa kuachiliwa kwa msamaha wakati wa janga la Covid-19 baada ya kushtakiwa kwa mauaji ya binti yake wa miaka 13 mnamo 2018.

Baadhi ya majimbo ya India yamewaachia wafungwa wengine katika jaribio la kuzuia msongamano wa watu kwenye magereza kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini Kumar alikuwa ameripotiwa kuwa ameshawishika kuwa mamlaka ilikusudia kumaliza kipindi chake cha msamaha na walipanga mpango wa kuepusha kufungwa kwake tena.

Polisi wanadai kuwa Kumar alikiri alipokamatwa na kumuua Domen Ravidas tarehe 19 Novemba.

Bw Ravidas alikuwa na urefu na uzito sawa na Kumar, ambaye alikuwa ameajiri mkandarasi kufanya kazi ya ukarabati wa nyumba yake.

Mwili wa Bw Ravidas uligunduliwa kwenye shamba lililokuwa wazi siku iliyofuata.

Mabaki yake yalichomwa kiasi cha kutotambulika, lakini alikuwa amebeba kitambulisho cha Kumar mfukoni mwake.

Mke wa Kumar, Anupama, baadaye aliutambua mwili huo kuwa wa mumewe nyumbani kwao katika mji mkuu wa India wa Delhi.

Hatahivyo, baada ya kubaini kuwa Kumar alighushi kifo chake, maafisa walipokea taarifa kwamba alikusudia kumtembelea mke wake.

Polisi walivamia nyumba ya wanandoa hao na kumkamata Kumar, ambaye alikiri kufanya uhalifu huo.

Mkewe pia amekamatwa kwa sehemu yake katika njama hiyo.

Iraj Raja, msimamizi wa polisi wa mkoa, alisifu kazi ya maafisa wake wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumapili.

"Wanandoa hao walipanga njama ya kina, lakini polisi walifanikiwa kukabiliana na kisa hiki cha mauaji," Bw Raja alisema. "Timu hii itatunukiwa kwa kazi yake," aliongeza.