Koffi Olomidé afutiwa kosa la ubakaji lakini ahukumiwa kwa kuwazuilia wacheza densi

Olomidé ameagizwa kuliwalipa wachezaji densi hao wanne dola 11,300 (£8,500) kila mmoja

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Olomidé ameagizwa kuliwalipa wachezaji densi hao wanne dola 11,300 (£8,500) kila mmoja

Mahakama ya rufaa nchini Ufaransa imemuondolea mwanamuziki Koffi Olomidé kosa la unyanayasaji wa kingono, lakini ikamtia hatiani kwa kuwashikilia wanawake bila hiari yao.

Mahakama ilibatilisha uamuzi wa 2019 uliompata na hatia ya ubakaji wa mmoja wa wachezaji densi alipokuwa na umri wa miaka 15.

Lakini alipatikana na hatia ya kuwanyima wanawake uhuru wao katika jumba la kifahari huko Paris kati ya 2002 na 2006.

Atatumikia kifungo cha miezi 18 kilichoahirishwa kwa muda na kuwalipa fidia.

Mwendesha mashtaka ya umma alikuwa amependekeza ahukumiwe kifungo cha chini ya miaka minane.

Watuhumiwa wake "bila shaka hawakuridhishwa na hukumu ya unyanyasaji wa kingono kwa sababi kwa hili lilikuwa kitu cha muhimu zaidi ", alisema wakili David Desgranges ambaye alikuwa akiwawakilisha wanawake hao.

Mmoja wao alikuwa amedai kuwa aliwashambuliwa "katika mahoteli, wakati mwingine ndani ya gari... na katika studio za kurekodi muziki".

Mahakama mjini Versailles haikumpata na hatia ya unyanyasaji wa kingono, huku jaji akifutilia mbali shtaka la ubakaji kutokana na "kubadilika na wakati mwingine kukinzana" kwa ushahidi kutoka kwa waliomtuhumu.

Hata hivyo mahakama iligundua kuwa kitendo chake dhidi ya wanawake hao "kiliwanyima uhuru kwa kuwekwa chini ya uangalizi wa mara kwa mara " na washirika wake wawili ambao waliwazuilia kwenye chumba wakiwa wamefungwa nyuso zao.

Mbali na adhabu hiyo iliyosimamishwa aliamriwa kulipa faini ya euro 10,000-32,000 ($11,000-36,000) kwa kila mcheza densi.

Olomidé, ambaye jina lake halisi ni Antoine Agbepa Mumba, ni mmoja wa wanamuziki maarufu zaidi barani Afrika.

Msani huyo mwenye umri wa miaka 65 ni nyota mkubwa wa muziki wa rumba na soukous ambayo ni maarufu sana Afrika. Mojawapo ya vibao vilivyopendwa zaidi katika kazi yake ya muda mrefu ni Loi ya 1997.

Mwimbaji huyo amekabiliwa kisheria mara kadhaa hapo awali:

  • Mwaka 2018 Zambia iliamuru kukamatwa kwake baada ya kudaiwa kumshambulia mpiga picha.
  • Mwaka 2016 alikamatwa na kurejeshwa njumbani baaada ya kuwashambulia wacheza densi wake nchini Kenya.
  • Mwaka 2012 alipatikana na hatia nchini DR Congo kwa kosa la kumshambulia mtayarishaji wake na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela.
  • Mwaka 2008 alituhumiwa kwa kumpiga teke mpiga picha wa kituo cha televisheni cha kibinafsi cha RTGA nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini baadaye wawili hao walipatana.