Waridi wa BBC: Abby Chams azungumzia changomoto za wanamuziki wa kike

  • Anne Ngugi
  • BBC Swahili
Abigail Chamungwana

Chanzo cha picha, Abigail

Maelezo ya picha,

Abigail Chamungwana

Akiwa na miaka 18 tu Abigail Chamungwana maarufu Abby Chams anaendelea kuimarika zaidi . Ni msichana ambaye nyota yake inazidi kung'aa .Lakini kisichojulikana ni kwamba msanii huyu amepitia mahangaiko , pandashuka na changamoto.

Anasema amepitia changamoto katika harakati zake kama msanii wa kike hasa katika mchakato wa uandishi wa muziki, kurekodi na kuhakikisha kwamba wimbo wake unasikizwa na umma.

"Ukweli mimi kama mwanamuziki kwenye sekta hii zipo changamoto , unajua nina miaka 18 Tu na unajua ninafanya kazi na watu wengi , Wazalishaji na waelekezaji ni wakubwa sana kwangu- ni kama wazee , wananitongoza, Yaani wananiweka kwenye hali ambayo sio nzuri ", anasema

Abby anasema kwamba kwa miaka mingi tangu aanze safari ya muziki amekabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutongozwa na watayarishaji wa muziki na waelekezi wa video .

Chanzo cha picha, Abigail

Maelezo ya picha,

Msanii huyu anasema kwamba ni tabia iliomkera sana hadi kulazimika kukata uhusiano wa kibiashara na baadhi ya watu aliokuwa akifahamiana nao.

''Hayo mambo yapo unakuta muelekezi umemfanyia kila kitu lakini anakataa kukupa video kwasababu amesema anakupenda na umemjibu kwamba hii ni biashara. Yani ni sawa , lakini mimi najua kama ni hivyo basi ni sawa .Unajua kwamba ninaweza kupata muelekezi wa video mwengine, ni kujiamini na kujua thamani yako".

Nyota huyu anakumbuka miaka ya hapo awali ambapo alikuwa anaelezwa kwamba ili watoe video za muziki wake baadhi ya waelekezi na watayarishaji wa muziki wake walimuweka katika njia panda kuhusu mahitaji yao, lakini yeye alikataa .

Chanzo cha picha, Abigail

Maelezo ya picha,

Sasa nilikuwa na uoga wakati wa mwanzo kuzungumzia hali hii na wazazi pamoja na jamii yangu

Abby anasema kwamba alifaulu kukwepa mitego hiyo kutokana na misimamo yake kuhusu Maisha. Kwa mfano anasema kwamba alijiwekea viwango vya Juu vya nidhamu mbele ya kupata umaarufu, pamoja na kuwa na wazazi waliomsitiri na kumyoosha.

Na hilo ndilo linalompa msukumo baada ya kufikisha umri wa kuingia katika utu uzima mwaka huu.

Hali kadhalika mwanadada huyu anasema kwamba amepoteza marafiki wengi wakati alipokuwa akijitenga kimziki.

Anasema kwamba baadhi ya rafiki zake wakati huo walionekana kuwa na muda wa kutangamana na kufanya mambo mengi ya ujana, Abby anakiri alipitia Sonona .

Chanzo cha picha, Abigail

"Kuna kipindi nimepitia sonona nikuwa na marafiki zangu, wote waliniacha na nilikuwa nashangaa ni kwanini wanaondoka.Walikuwa wanasema kwamba muda wangu mwingi nimeutengea ala za kimziki na masomo .Wao walitaka niwepo wanapotaka kujivinjari lakini sikuwa na nafasi hiyo'', anaongezea

Ila anajivunia hatua alizochukua kwa sasa, kwani ameibuka kuwa nyota aliyejijenga kielimu na kisanii .

Ameafikia nini haswa

Akiwa na umri wa miaka tisa tu, Abby Chams , tayari aliweza kucheza ala tatu za muziki - piano, violin na gita, wakati wote akijifunza akiwa na umri mdogo zaidi .

Kipaji hiki na mapenzi ya muziki ni kitu ambacho mwanamke huyu mchanga anaamini alizaliwa nacho, na kinatokana na uhusiano wa familia yake na muziki.

Chanzo cha picha, Abigail

Maelezo ya picha,

Hivi majuzi alitunukiwa tuzo ya muziki ya vijana wanaochipuka Tanzania

Anasema kwamba marehemu babu yake alikuwa mwanamuziki na kiongozi wa kwaya .Anajivunia uongozi wake katika fani ya muziki mbali na kuwa mwalimu wake wa kwanza wa piano alipofikisha umri wa miaka mitano.

Hivi majuzi alitunukiwa tuzo ya muziki ya vijana wanaochipuka Tanzania kwa sababu ya kazi yake ya kuwashirikisha vijana kupitia muziki.

Tuzo hiyo inajiri baada ya mwanadada huyo kutajwa kuwa mtetezi wa vijana na Unicef nchini Tanzania kuhusu Afya ya Akili na Usawa wa Jinsia wakati wa Siku ya Kimataifa ya Mtoto Duniani 2020. Pia alitoa wimbo kuashiria hafla hiyo.

"Haya ni masuala mawili ambayo ninayapenda sana, na nina heshima kufanya kazi na Unicef," aliiambia Wanahabari.

Anaamini Unicef ilimchagua kwasababu ya kazi ya utetezi ambayo tayari alikuwa akifanya kwa usawa wa kijinsia, masuala ya afya ya akili na vijana nchini Tanzania

Miaka miwili iliyopita, Abby alianzisha programu ya vijana "Teen Talks With Abby Chams", kama "mahali salama kwa vijana kuzungumza juu ya changamoto zinazowakabili na kujadili suluhu, kurekebisha masuala ya afya ya akili na kuondoa aibu na unyanyapaa unaoizunguka. ," alisema Abby Chams.

"Nakumbuka karibu niache muziki nikiwa darasa la tatu, lakini wakati huu nilijifunza kujisukuma kupita mipaka yangu, kuwa na nidhamu na motisha katika mazoezi yangu. Wazazi wangu pia walichangia sana katika kunitia moyo. Ninajivunia sana kwa kuvumilia na natumai mtu mwingine atatiwa moyo kuendelea kucheza au kufanya mazoezi atakaponiona nikicheza ala yangu ya muziki," aliongeza.

Chanzo cha picha, Abigael

Maelezo ya picha,

Abby ni kielelezo kwa wengi hasa vijana wa Tanzania na nchi za Kanda hii ya Afrika mashariki .

Vilevile Abby Chams alitajwa kuwa balozi Tanzanite Expo 2020 Dubai mwaka alipokea wa shida huo Ali ulikuwa kusema Haya :

Alisema kuwa anafarijika sana kuona nchi yake imesimama miongoni mwa nchi 192 ambazo zinashiriki katika maonesho haya ya Expo 2020 Dubai.

Amemaliza masomo yake ya shule ya upili na kufaulu kwa daraja la A .

Anapanga kusomea Biashara na Fedha chuoni.

Kichwa cha habari cha awali katika taarifa hii kiliashiria kwamba Abby Chams alisema kuwa aliahidiwa umaarufu iwapo angekubali kuwa katika mapenzi .

Tunaomba radhi kwa kosa hili