Dubai wakasirishwa na Kenya

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya yuko Dubai kutuliza mzozo uliopo baada ya wanafamilia wa taifa hilo walipofukuzwa kwa kushukiwa kuhusika na ugaidi.

Watu hao wanne kutoka Dubai walikuwa likizo na kukaa kwenye hoteli moja mjini Mombasa wakati wa Pasaka, baada ya maafisa wa uhamiaji kuwasaili kwa saa kadhaa kabla ya kuwafukuza.

Kutokana na hatua hiyo nchi hiyo iliyopo katika Falme za Umoja wa Kiarabu UAE imeamua kuweka sheria kali za kuwaruhusu Wakenya wenye shahada tu kuingia nchini humo.

Sheria hiyo mpya na kali imewaathiri wafanyabiashara wengi, ambao aghalabu hununua bidhaa zao kutoka Dubai.

Mwandishi wa BBC Ruth Nesoba wa mjini Nairobi amesema magari yaliyotumika na vitambaa kutoka Dubai ni biashara kubwa inayofanywa na wafanyabiashara kutoka Kenya.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Moses Wetangula na maafisa wenzake waliwasili UAE siku ya Jumatatu lakini walishindwa kuafikiana na hivyo mazungumzo hayo yameongezewa muda.

Wiki iliyopita, naibu waziri wa mambo ya nje Richard Onyoka aliomba radhi kwenye idhaa ya Kiswahili ya BBC kwa makosa waliyofanya maafisa wa polisi.

Kutokana na gazeti la Standard la Kenya takriban Wakenya 37,000 wanaishi UAE na hasa Dubai.