Matokeo murua kwa rais Bashir wa Sudan

Wanaomuunga mkono rais wanauchukulia ushindi huu kama jibu la wananchi wa Sudan kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ambayo imetoa kibali cha kukamatwa kwa bwana Bashir ikimtuhumu kwa uhalifu wa kivita katika Darfur.

“Huu ni ujumbe kwa dunia nzima: rais ni halali na ni mwakilishi wa watu wote,“ akasema ofisa wa NCP Rabie Abdelati.

“Mashtaka yoyote sasa ni mashtaka dhidi ya wananchi wote”

Hata hivyo Mahakama ya Kimataifa yaUhalifu (ICC) imesema kuwa matokeo hayo ya uchaguzi hayatabadilisha uamuzi wake wa kutaka kumshtaki Rais Bashir.

Ushindi wake wa 68% ulikuwa wa kusadikisha na chama chake kikajizolea ushindi mkubwa kaskazini.

Image caption Rais wa Sudan

Matokeo hayo yamepingwa na upinzani, na kutiliwa shaka na wengine, kufuatia shutuma nyingi za udanganyifu.

Lakini wakati kura ya maoni mwakani juu ya uwezekano wa Sudan ya kusini iliyo huru ikikaribia kwa kasi, chaguzi hizi zitakubaliwa kimataifa.

Wakati vyama kadhaa pinzani kwa Rais Bashir, kikiwemo waasi wa zamani wa SPLM ambao wanaongoza kusini, walipojitoa kwenye mbio za urais, walizidisha sana makadirio ya nguvu zao.

Msimamo wao imara uliathirika vibaya wakati baadhi ya vyama vilipoamua kushiriki.

‘Vitisho’

Wale waliopinga waliamini kuwa kujitoa kwao kuliondoa uhalali wote wa uchaguzi.

Wakaguzi wa kimataifa, kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Carter Centre, walishutumu chaguzi kuwa “hazikukidhi viwango vya kimataifa”.

Lakini kwa mshangao wa upinzani nchini Sudan, rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter aliweka wazi kabisa kuwa ‘jumuiya ya kimataifa’ itawatambua washindi wa uchaguzi.

Wanasiasa toka kambi ya upinzani kaskazini mwa nchi wanadai utaratibu mzima wa uchaguzi ulikuwa wenye mapungufu, ikiwemo uanishaji wa majimbo, sensa, uandkishaji wa wapiga kura na uchaguzi wenyewe.

Wakaguzi kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu na Umoja wa Afrika wamesisitiza kuwa chaguzi zilikuwa za haki na huru.

Image caption Salva Kiir, Rais wa Sudan Kusini

Baadhi ya wakaguzi kutoka Sudan wanapinga vikali.

Sudan Democracy First, jumuiya mama kaskazini mwa nchi, ilitoa kile ilichokiita ushahidi mkubwa wa udanganyifu uliofanywa na chama cha Rais Bashir (National Congress Party).

Shirika la Mtandao wa Demokrasia na Uchaguzi (Sunde) lilisema kulikuwepo na udhalilishaji na vitisho kusini mwa nchi kutoka kwa majeshi ya SPLM.

Katika maeneo yote ya nchi hii iliyogawanyika, raia wa kawaida na wagombea ambao hawakuridhika walijihatarisha kwa kuainisha mambo mabaya yaliyofanyika katika chaguzi.

Maswali yanayoleta wasiwasi

Filamu ya siri inayoonesha maofisa wa uchaguzi mashariki ya Sudan wakifanya udanganyifu katika uchaguzi kwa ajili ya chama cha NCP iliwekwa katika mtandao wa YouTube.

Majeshi yanayomilikiwa na SPLM kusini mwa Sudan yalishutumiwa kwa kutesa watu ambao hawakupigia kura SPLM.

Wagombea pinzani dhidi ya SPLM wanasema kuwa ama walitiwa kizuizini au kuzuiwa kupiga kampeni.

Ikiwa sehemu ya shutuma hizi zitakuwa na ukweli basi inaacha maswali mengi ya kutia wasiwasi juu ya kura ya maoni, na hasa namna Kusini itakavyotawaliwa ikiwa itakuwa huru.

Hivyo basi hali hii ya mvutano inaipeleka nchi wapi?

Sudan Kaskazini kuliko wakati wowote ule iko katika himaya ya Rais Bashir na chama chake, ambacho kilishinda kila kiti ilichogombea, zaidi ya yale maeneo yenye mvutano katika mpaka wa kasakazini-kusini.

Inavyoonekana ni kuwa Rais Bashir ameimarisha himaya yake kabla ya kura ya maoni mwezi wa kwanza mwakani juu ya uwezekano wa kusini iliyo huru.

Kupoteza imani

Maofisa kutoka katika chama chake wameeleza kuwa wataendelea kutoa ule ule uhuru wenye mipaka kama ilivyokuwa wakati wa kampeni za chaguzi.

Lakini wengi wana mashaka.

Upinzani kaskazini umeyashutumu matokeo na kudai hautakubali matokeo na kutaka maandamano ya amani kufanyika ili kudai chaguzi mpya.

Hata hivyo, Rais Bashir ana mamlaka, yawe ya kidemokrasia au vinginevyo kufanya apendavyo.

Upinzani mkali pekee unatolewa na SPLM kusini mwa nchi.

Chenyewe pia kilipata ushindi mkubwa katika maeneo kinayomiliki. Kwa mfano, katika viti kumi vya magavana wa majimbo kiliweza kushinda viti tisa.

Kiti cha kumi cha ugavana kilikwenda kwa mgombea binafsi-ambaye ni kanali wa jeshi katika SPLA kusini.

Mrejesho wa wanasiasa wa kusini waliopoteza matumaini, wakiwemo wagombea binafsi walioshindwa ni muhimu kuutazama.

Upande mmoja kujitenga?

Baada ya kujiimarisha, wote kaskazini na kusini wanaelekeza macho yao sasa kwenye kura za maoni.

Rais Bashir, kwa mara nyingine tena, alisisitiza katika hotuba iliyotangazwa punde baada ya matokeo kutangazwa, nia yake ya kuhakikisha kura ya maoni inafanyika kwa wakati.

Lakini wengi kusini wana mashaka.

“Nina wasiwasi sana kuwa Nationa Congress katika miezi ijayo watajaribu kuchelewesha kura ya maoni” akasema Yassir Arman wa SPLM ambaye alipata kura zaidi ya milioni mbili kwa nafasi ya urais, licha ya kwamba alijitoa katika uchaguzi.

SPLM kimeshatangaza wazi kabisa kuwa ikiwa kura ya maoni itacheleweshwa kitatoa uamuzi wa upande mmoja wa kutangaza uhuru.

Hivyo baada ya uchaguzi kukamilika ni wakati wa majadiliano mengi magumu.

Kwanza, Rais Bashir ataunda serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo lazima ijumuishe SPLM, lakini labda si wapinzani wengi watakuwemo humo.

Baada ya hapo NCP na SPLM lazima wakubaliane juu ya mambo kadhaa muhimu kuhusu kura ya maoni, ikiwemo labda pia jambo zito la kutengwa kwa mpaka wa kaskazini-kusini.

Hatimaye, uchaguzi wa Sudan huenda ukaonekana tu kama hatua yenye dosari kuelekea kura ya maoni.