Brown akwaa kisiki cha kampeni Uingereza

Kampeni ya Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, imekwaa kisiki baada ya kinasa sauti kurekodi mazungumzo yake akimwelezea mpiga kura mmoja kuwa mwenye kushikilia itikadi au 'king'ang'anizi'.

Bw Brown ametumia muda mwingi kuomba radhi, lakini ni wazi kuwa maneno yake mwenyewe yamezidi kudidimiza kampeni yake ambayo tayari ilionekana kuzidiwa nguvu na wapinzani wake wa Conservative na Liberal Democrats.

Image caption Bw Brown alikasirishwa na maswali ya Bi Duffy aliyelalamikia uwingi wa wageni kutoka Ulaya Mashariki.

Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari, Bw Brown alieleza kuwa "amedhalilika" baada ya maneno aliyotoa kumwelezea Bi Gillian Duffy, mwenye umri wa miaka 65, ambaye alitaka kupata majibu kutoka kwa kiongozi huyo kuhusu maswala ya uhamiaji.

Wakati alipoingia kwenye gari yake, alikuwa bado amevaa kinasa sauti cha kurushia matangazo ndani ya koti, ndipo aliposikika akisema "sikufahia kuongelea swala lile".

Kuomba radhi

Baadaye Bw Brown alizuru nyumbani Bi Duffy katika mji wa Rochdale kwenda kuomba radhi na kisha akawatumia barua pepe wanaharakati wa chama cha Labour na kusema anajutia maneno yake.

Baada ya kuzungumza na Bi Duffy kwa zaidi ya dakika 40, Bw Brown alijitokeza na kusema: "Unaweza kusema najuta kutenda dhambi. Kuna wakati unasema vitu usivyomaanisha kuvisema, wakati mwingine unasema vitu kwa bahati mbaya na wakati mwingine unaongea vitu utakavyotaka kurekebisha haraka kadri iwezekanavyo.

"Nilitaka kuja hapa kumwambia Gillian samahani, nilifanya kosa, lakini pia nasema naelewa dukuduku alilokuwa akinieleza na sikumwelewa vyema baadhi ya maneno aliyonieleza."

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema hilo ni pigo kubwa kwa Bw Brown ambaye tayari kura za maoni zilikuwa zikionyesha kuwa anakabiliwa na mlima mrefu wa kuwazidi nguvu wapinzani wake David Cameron wa chama cha Conservative na Nick Clegg wa Liberal Democrats.