Afisa wa misaada wa UN azuru Congo

Ramani ya Mashariki mwa DRC

Afisa mkuu wa shughuli za dharura wa Umoja wa Mataifa amezuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku makundi ya waasi wenye silaha yakiendelea kuteteresha usalama.

John Holmes atatembelea majimbo matatu ambako wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanakabiliwa na mazingira magumu ya kazi.

Pia atazuru jimbo ambako maelfu ya watu inasemekana wamekimbia makazi yao kuepuka mapigano.

Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile ubakaji na uporaji vimekuwa vikijitokeza kwa kiasi kikubwa nchini humo.

Mapigano na ujambazi

Bw Holmes atazuru jimbo la Kivu, ambako shughuli za kijeshi zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuwasaka waasi wa kihutu kutoka Rwanda, zimesababisha maelfu ya wakazi kukimbia.

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanasema ahadi ya usalama wa raia ilitolewa baada ya shughuli kama hiyo iliyofanyika mwaka jana, ingawa hali bado ni mbaya.

Na wanasema, hali ya raia kuhamahama limekuwa ni jambo la kawaida. Misaada inakuwa vigumu kuwafikia walengwa kutokana na mapigano na ujambazi.

Bw Holmes pia atasafiri kwenda kaskazini-mashariki ya nchi hiyo, ambako waasi wa LRA kutoka Uganda bado wanaendelea kusumbua wanavijiji.