Mdahalo wa mwisho wa viongozi Uingereza

Viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini Uingereza wakiwa katika mdahalo wa mwisho.
Image caption Ilikuwa ni fura ya mwisho kwa Cameron, Clegg na Brown kujinadi kabla ya uchaguzi wiki moja ijayo.

Katika mdahalo wa mwisho kuwapambanisha viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini Uingereza uliofanyika Alhamis usiku, Waziri mkuu wa sasa, Gordon Brown, alitumia fursa hiyo kuwaomba wapiga kura wasifanye makosa kubadilisha serikali inayoongozwa na chama cha Labour.

Kiongozi huyo wa chama cha Labour, ambaye chama chake kipo nafasi ya tatu kwa mujibu wa kura za maoni, alionya uwezekano wa chama cha Conservative kuunda serikali ya mseto na chama cha Liberal Democrat, akisema kwa kufanya hivyo mipango ya kufufua uchumi wa nchi itaathirika.

David Cameron alimlaumu Bw Brown kwa kujaribu "kuwatisha" wapiga kura akaeleza kuwa chama chake cha Conservative kitaleta mabadiliko yanayohitajika.

Nick Clegg aliwasihi wapiga kura "kuchagua mustakabal wanaoutaka kwa uhakika".

Ushindani

Mhariri wa BBC wa maswala ya kisiasa, Nick Robinson, amesema mdahalo haukuwa na mshindi wa wazi, lakini baada ya matukio ya siku ya Jumatano, Bw Cameron ameonekana kunufaika na kujijengea nafasi kubwa ya kupata ushindi.

Mtaalam wa BBC wa maswala ya kura za maoni, David Cowling, amesema aina mbili za kura za maoni zilizofanywa wakati wa mdahalo zikiendeshwa na ComRes na YouGov, zimeonyesha mtizamo unaofanana - Bw Clegg yuko nafasi ya pili kama ilivyokuwa mdahalo wa pili, Bw Cameron amepata ongezeko la asilimia nne na Bw Brown ameporomoka asilimia nne.

Katika mdahalo huo uliosimamiwa na BBC mjini Birmingham, viongozi hao walijadili maswala kama sera za uchumi, uhamiaji, makazi, mageuzi ya kisiasa, elimu, kodi, mageuzi ya sekta ya benki na mipango ya kubana matumizi.

Bw Brown alikuwa na chagizo la kufufua kampeni ya Labour, ambayo siku ya Jumatano ilipata pigo kutokana na kiongozi huyo kumsema vibaya mpiga kura aliyemwuliza maswali magumu kuhusu ongezeko la wahamiaji, alilazimika kumwomba radhi.