Museveni kujieleza mbele ya tume

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekubali kufika mbele ya tume ya uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za maandalizi ya mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Taarifa kutoka ikulu ya rais imethibitisha Rais Museveni kupangiwa kukutana na tume hiyo wakati wowote.

Uganda iliandaa mkutano wa wakuu wa mataifa ya Jumuiya ya Madola (CHOGM) mwaka 2007 na kuhudhuuriwa kama kawaida na Malkia Elizabeth wa pili ambaye ni mkuu wa jumuiya hiyo.

Image caption Rais Museveni ameapa kuadhibu yeyote atakayepatikana na hatia

'Rais aliruhusu'

Tume hiyo inachunguza madai kwamba fedha nyingi zilitumika vibaya kuandaa mkutano huo, ambapo rais Museveni anadaiwa kukubali matumizi zaidi kuliko fedha zilizotengwa kwa ajili ya mandalizi hayo.

Madai mengine katika sakata hilo ni matumizi ya dola milioni tano kununua vyombo vya mawasiliano, badala ya dola milioni tatu zilizoidhinishwa awali. Watu waliohojiwa na tume hiyo wamedai kuwa rais aliruhusu hatua hiyo.

Ununuzi wa magari

Aidha rais Museveni anatazamiwa kutolea maelezo madai ya fedha nyingi kutumika katika mahoteli na ununuzi wa magari.

Katika hotuba yake kwa taifa kwenye mkesha wa mwaka mpya, rais Museveni, ambaye ndiye ametaka kuwepo kwa tume hiyo, aliapa kuadhibu afisa yeyote wa serikali ambae atapatikana na hatia ya kutumia vibaya pesa za CHOGM.

Tume hiyo inakamilisha kazi yake, na kabla ya kufanya hivyo pia ilitaka kukutana na rais.