Makamu Rais wa Uganda matatani

Uchunguzi uliofanywa na bunge la Uganda kuhusu matumizi mabaya ya fedha za serikali umependekeza kuwa Makamu wa Rais, Gilbert Bukenya, na mawaziri kadhaa na mawaziri kadhaa wanatakiwa kufunguliwa mashtaka.

Madai dhidi yao yanatokana na zabuni za serikali zilizotolewa kwa ajili ya mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Uganda mwaka 2007.

Image caption Gilbert Bukenya, makamu wa Rais wa Uganda anakabiliwa na tuhuma nzito za ubadhirifu.

Uchunguzi uliofanywa na bunge la Uganda kuhusu matumizi mabaya ya fedha za serikali umependekeza kuwa Makamu wa Rais, Gilbert Bukenya, na mawaziri kadhaa wanatakiwa kufunguliwa mashtaka.

Kamati ya bunge ya mahesabu ya umma imedai kuwa Bw Bukenya alikiuka taratibu katika kuagiza magari maalum ya kutumiwa na viongozi wakati wa mkutano huo. Siku ya Alhamisi, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliitwa mbele ya bunge kujitetea. Haijajulikana aliongea nini, lakini lengo lilikuwa kubaini endapo naye alihusika na kashfa hiyo.

Ripoti ya awali ya kamati hiyo ya bunge inasema, Makamu wa Rais Gilbert Bukenya ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya mawiziri iliyokuwa inapanga mkutano huo alikiuka sheria za kutoa zabuni na lazima awajibike.

Tuhuma nzito

Kamati hiyo ya bunge iliyoidhinishwa na Rais Museveni inasema kulikuwepo na udanganyifu katika utoaji wa zabuni kwa watu binafsi na makampuni yaliyotoa huduma wakati wa mkutano huo wa Jumuiya ya Madola uliosababisha serikali kupoteza mamilioni ya dola.

Wana kamati wanasema hatua ya Makamu wa Rais Bukenya ya kukiuka sheria inabainisha jinsi serikali ilivyoonyesha ujeuri na wamesikitika kuwa alikataa kufika mbele yao kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.

Mawaziri wengine waliojikuta matatani baada ya uchunguzi huo ni yule wa mambo ya nje, wa utalii vile vile barabara na ujenzi.