Takriban watu 20 wafa maji Tanzania

Zaidi ya abiria 20 wanahofiwa kufa maji katika mkoa wa Mtwara kusini mwa Tanzania kutokana na ajali ya boti ambayo haijajulikana jina lake.

Boti hiyo ambayo inakadiriwa kuwa na watu 28 imezama leo mchana katika bahari ya Hindi.

Awali mwandishi wetu Josephat Mwanzi alizungumza na kamanda wa polisi wa Mtwara Steven Buyoya aliyekuwepo kwenye eneo la tukio akisema watu wanane wameokolewa lakini mmoja miongoni mwao amefariki dunia.

Image caption Boti, Tanzania

Wakati kazi ya uokoaji ikiendelea, mmiliki wa boti hiyo ambaye hajajulikana mpaka sasa amekimbia pamoja na kapteni wake.

Boti hiyo kutokana na kamanda Buyoya ina uwezo wa kubeba abiria 18 lakini pia hujikuta ikijaa kutokana na mizigo zikiwemo basikeli.

Boti hiyo inayomilikiwa na mtu binafsi aghlabu hubeba wavuvi na wachuuzi wadogo wadogo.

Shughuli ya kuokoa watu hao imesitishwa kutokana na kiza na itaendelea siku ya Jumamosi saa mbili asubuhi.