Mafuta yatishia mazingira Marekani kusini

Mfanyakazi akiweka maboya kuzuia mafuta yasisambae Ghuba ya Mexico, Marekani.
Image caption Mfanyakazi akiandaa maboya kuyatandaza baharini kuzuia mafuta yasisambae Ghuba ya Mexico, Marekani.

Jeshi la Marekani limeungana na jitihada za kuzuia mafuta yanayovuka kutoka kisima kimoja yasisambae katika Ghuba ya Mexico, huku wasi wasi ukiongezeka kuhusu zitakazojitokeza.

Kiasi cha mafuta mara tano zaidi ya ilivyokadiriwa awali huenda yakawa yanavuja kutoka kwenye kisima ambako mtambo wa kuchimbia mafuta ulilipuka na kuzama juma lililopita, Idara ya usalama wa pwani ya Marekani imeeleza.

Rear Admiral Mary Landry amesema inakadiriwa kuwa kiasi cha mapipa 5,000 ya mafuta yanamwagika kuingia baharini katika eneo la Louisiana.

Udhibiti

Wizara ya usalama wa ndani ya Marekani imetaja tatizo hilo kuwa ni jambo la umuhimu wa kitaifa.

Waziri wa usalama wa ndani, Janet Napolitano, ambaye atakuwa Louisiana kusimamia shughuli hizo, aliwaeleza waandishi wa habari mjini Washington kuwa hatua hiyo itatoa fursa ya usaidizi kuagizwa kutoka sehemu nyingine za Marekani.

Wakati huo huo, serikali ya Marekani imeagiza ukaguzi wa visima vyote virefu katika Ghuba ya Mexico kuona endapo sheria za kudhibiti kuvuja kwa mafuta zinazingatiwa.

Kuna wasi wasi mkubwa kuwa mafuta hayo yataathiri mazingira, wanyama na mimea. Watu wengi watakosa kipato hasa wavuvi na wale wanaotegemea biashara ya utalii baharini.