LRA wafanya mauaji mapya Kongo

Umoja wa Mataifa unachunguza ripoti za mauaji yaliyofanywa na waasi wa Uganda huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afisa mwandamizi wa umoja huo amesema takriban watu 100 wameuawa katika shambulio linalodaiwa kufanyika, na kuaminiwa kufanywa mwezi Februari.

John Holmes, mkuu wa umoja huo wa masuala ya kibinadamu, amesema akiwa ziarani Kongo kwamba uchunguzi unafanywa.

Iwapo madai hayo yatathibitishwa idadi ya watu watakaokuwa wameuawa baina ya mwezi Desemba na Machi watafikia 500.

Bw Holmes amesema waasi wa Lords Ressitance Army LRA walihusika na mauaji hayo katika kijiji cha Kapanga kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, karibu na mpaka wa Sudan kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Baada ya kuzuru kijiji cha Niangara, karibu na eneo linalodaiwa kufanywa mauaji hayo, Bw Holmes amesema uchunguzi umeanza ili kujua hasa kilichotokea.

Umoja wa Mataifa unasema kipindi hicho hicho, wengine 300-nusu yao wakiwa watoto- walitekwa. Idadi isiyojulikana ya wanakijiji nao walikatwa viungo, kulingana na umoja huo.

Miongoni mwao ni Marie Mbolihundele, anayesema alitekwa na waasi watatu wa LRA kaskazini mwa eneo la Niangara wiki mbili zilizopita. Anasema walimkata midomo na sikio lake moja.

Alisema, "Waliamuru nilale sakafuni na waliniambia nisipige kelele au wataniua."

"Nikaanza kuswali, kisha wakavuta midomo yangu na kibanio na kuikata na kisu. Kisha wakaniambia nikimbie, kwahiyo nikasimama na kukimbia."

Bw Holmes amekiri kwamba majeshi ya Kongo na Uganda waliosambazwa eneo hilo kuwasaka waasi wa LRA wamefanikiwa kwa kiasi fulani.

Lakini waasi hao kwa sasa wameenea sehemu kubwa na kusababisha hofu kubwa, amesema Bw Holmes.

LRA ilianzishwa nchini Uganda mwaka 1987 kwa nia ya kuipindua serikali. Harakati hizo ziliisha mwaka 2005, lakini waasi wakaanza kuwashambulia wanakijiji huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.