Waasi wa Darfur wasusia mazungumzo

Kundi kubwa zaidi la waasi katika eneo la Darfur Magharibi mwa Sudan limesusia mazungumzo kati yake na serikali wakiilaumu kwa kuanzisha upya mashambulizi.

Image caption Waasi wa Darfur

Kundi la Justice and Equality Movement linasema jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi ya ngani vijijini kinyume na makubaliano ya mwezi Februari.

Hatahivyo msemaji wa jeshi amesema majeshi hayo yalichukua hatua hiyo baada ya kushambuliwa. Inahofiwa kuwa huenda hatua hiyo ikachochea mapigano kuanza upya katika eneo hilo la Darfur na kuhatarisha wakaazi ambao wengi wameachwa bila makao kutokana na mzozo wa muda mrefu.

Image caption Wakimbizi wa Darfur

Kiongozi mmoja wa kundi la Jem Ahmed Tugod Hassan ameiambia BBC kuwa mapigano hayo ya hivi karibuni yametokea katika eneo la Jebel Moon Magharibi mwa Darfur.

Hata hivyo, msemaji wa serikali amewalaumu waasi na kuwataja kama chanzo cha kuvunjika makubalino ya kusitisha mapigano.

Waasi hao wamesema hawako tayari kurejelea mazungumzo hadi pale wajeshi wa Sudan watakapositisha mashambulizi.

Msemaji wa kundi hilo Ahmed Hussein Adam amesema kundi hilo limejiondoa kabisa katika mazungumzo ya Doha.

Mapigano hayakutokea katika eneo la Darfur wakati wa uchaguzi wa mwezi Aprili ambapo Rais Omar al-Bashir alijipatia ushindi. Lakini uchaguzi haukufanyika katika maeneo mengi ya Jimbo la Darfur kwa hofu ya usalama.

Rais Bashir anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, madai ambayo amekanusha.

Tangu mzozo wa Darfur kuanza mwaka 2003,watu millioni 2.7 wamelazimika kuyahama makaazi yao na Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya 300,000 wameuawa.

Makundi ya waasi yamekuwa yakipigana na wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa Kiarabu ambao watu wengi husema wanaungwa mkono na serikali.