Mtuhumiwa wa ugaidi Marekani ashtakiwa.

Raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Pakistan ameshtakiwa kwa makosa ya ugaidi na kujaribu kutumia silaha za maangamizi katika shambulio la bomu lililotegwa katika gari, ambalo lilitibuka.

Maafisa wa Marekani wamesema Faisal Shahzad, 30, amekiri kupata mafunzo ya kutengeneza mabomu nchini Pakistan.

Bw Shahzad alikamatwa akiwa ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea Dubai, katika uwanja wa ndege wa JFK mjini New York, siku mbili baada ya bomu hilo kugundulika.

Awali, rais Barack Obama aliwaahidi wananchi wa Marekani kuwa hawata tawaliwa na hofu kwa sababu ya tukio la Times Square.

Bw Obama alisema, "tukio hilo ni kumbusho la nyakati tunazoishi na lazima haki itendeke".

Inaaminika Faisal Shahzad alinunua gari aina ya SUV ambayo ilipatikana imesheheni bomu zilizotegenezewa nyumbani.

Licha ya jina lake kuongezwa katika orodha ya watu wasio takiwa kusafiri, Jumatatu iliyopita, Bw Shahzad aliweza kununua tiketi katika shirika la ndege la Emirates na kufanikiwa kupita vizuizi vya ukaguzi vya usalama katika uwanja wa JFK.

Familia ya mtuhumiwa huyo inasemekana kutoka mji ulioko kaskazini mwa Pakistan wa Peshawar, karibu na ngome na viwanja vya mafunzo ya ugaidi ya kundi la Taleban.

Habari kutoka Pakistan zinasema kuwa bw Shahzad alioa miaka miwili iliyopita kutoka mji wa Peshawar. Mke na mtoto wake mmoja wanaishi na jamaa katika mji wa Karachi.