Mgomo watatiza shughuli Ugiriki

Maelfu ya waandamanaji wameanza kukusanyika katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens, katika mgomo kupinga mpango wa serikali kuunusuru uchumi wa nchi hiyo.

Mgomo huu wa kitaifa ni wa tatu katika miezi michache iliyopita.

Safari zote za ndege nje na kuingia nchini humo zimesimamishwa. Bei za hisa barani Asia pia zimeanguka kutokana na hofu kuwa msukosuko wa kiuchumi wa Ugiriki huenda ukaathiri kanda inayotumia sarafu ya Euro.

Waandamanaji wamesema wanaadhibiwa kwa makosa ambayo hawakufanya. Maelfu tayari wamewasilisha barua za kustaafu wakitumaini kupata malipo ya uzeeni kabla ya sheria mpya kupitishwa. Sheria hiyo inapunguza malipo hayo au kuyasimamisha kabisa.

Serikali imekuwa ikiwashawishi wafanyikazi kutostaafu ikihofia kushindwa kukimu malipo hayo wakati tayari imeshindwa kukithi bajeti ya kitaifa.

Mpango wa serikali kupunguza matumizi yake ni mojawapo ya masharti yaliyowasilishwa na shirika la fedha duniani pamoja na Jumuiya ya Ulaya kwa Ugiriki kabla ya kupewa mkopo kusaidia kuuchepua uchumi wake.