Rais Yar'Adua wa Nigeria afariki Dunia

Rais wa Nigeria Umaru Yar'Adua amefariki katika makazi maalum ya rais kufuatia kuugua kwa muda mrefu.

Image caption Rais Umaru Yar'Adua aliingia madarakani mwaka 2007

Serikali ya Nigeria imetangaza siku saba za maombolezo, na kusema rais huyo atazikwa siku ya Alhamisi.

Makamu wa Rais, Goodluck Jonathan, ambaye ndiyo ameshika madaraka ya nchi tangu mwezi Februari mwaka huu, anatazamiwa kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo, kwa mujibu wa maafisa nchini humo.

Rais Yar'Adua mwenye umri wa miaka 58, aliingia madarakani mwaka 2007 na kuahidi kuleta mabadiliko mengi. Wachambuzi wa mambo wanasema alipiga hatua kubwa katika kutatua mzozo katika eneo lenye mafuta mengi la Niger Delta.

Kituo cha televisheni cha taifa kilikatiza matangazo yake ya kawaida kutangaza taarifa hizo mapema siku ya Alhamisi.

Mtangazaji alisema"Rais na amiri jeshi mkuu Umaru Musa Yar'Adua amefariki dunia saa chache zilizopita katika makazi ya rais".

Mtangazaji huyo akaendelea kusema "Maafisa usalama walimjulisha mshauri wa usalama wa taifa Jenerali Anou Bissou ambaye mara moja alimtaarifu kaimu rais. Marehemu alikuwa akiugua kwa muda.

Rambirambi

Muda mfupi baada ya kifo cha rais Yar'Adua kutangazwa, watu walianza kuwasili katika makazi maalum ya rais mjini Abuja kutoa rambirambi zao. Bw Yar'Adua anazikwa katika jimbo la Katsina, kaskazini mwa Nigeria.

Msemaji wa Bw Jonathan amesema kaimu rais huyo amepokea taarifa hizo kwa "mshituko mkubwa na masikitiko.

"Nigeria imepoteza lulu yake, na hata mbingu zinaomboleza na taifa letu" amesema Bw Jonathan kupitia taarifa. Kaimu rais huyo ametangaza siku ya Alhamisi kuwa ya mapumziko na mwanzo wa maombolezo.

Rais wa Marekani Barack Obama ameongoza kuwasilisha salaam za rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani.