Wasifu wa Umaru Yar'Adua

Umaru Musa Yar'Adua aliapishwa kushika hatamu za uongozi mwezi wa Aprili mwaka 2007 na kuwa kiongozi wa 13 wa Nigeria. Kabla ya hapo marehemu alikuwa ametangazwa mshindi kwenye uchaguzi uliozua ubishi mkubwa kutoka upinzani, kutokana na hali ya kutatanisha iliyotangulia kutangazwa matokeo hayo.

Image caption Marehemu Yar'Adua

Bw Yar'Adua alikuwa chaguo la mtangulizi wake Olusegun Obasanjo kuwa mgombea wa chama tawala cha Peoples Democratic Party, na wadadisi wengi waliona hilo kama jaribio la Bw Obasanjo kuendelea kuhodhi mambo hata baada ya kustaafu.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Ngeria kwa kiongozi aliyechaguliwa na raia kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine wa kuchaguliwa na raia, baada ya kukumbwa na miongo mitatu ya utawala wa kijeshi.

Kipindi kifupi cha marehemu Umaru Musa Yar'Adua cha Urais wake kiligubikwa na kudhoofika afya yake. Kwa zaidi ya miaka kumi Bw Yar'Adua alikuwa akikabiliwa na matatizo ya figo, na baadaye akakumbwa na maradhi ya moyo. Hata wakati wa kampeni za uchaguzi gumzo lilikuwa likiendelea kuwa hali yake ya afya haikuwa njema na siku chache kabla ya uchaguzi alisafirishwa kwenda Ujerumani kwa matibabu.

Hali mbaya ya afya ilimfanya Bw Yar'Adua kwenda kwa kasi ndogo kutekeleza ahadi saba alizotoa baada ya kuchaguliwa. Tofauti na mtangulizi wake Bw Obasanjo ambaye alikuwa mchapa kazi, Yar'Adua alikuwa akifanya kazi kwa muda usizodi saa nne kwa siku. Kutokana na mwendo huo wa pole wa utekelezaji wa majukumu yake Wanigeria wenyewe wakambandika jina Baba Go Slow- yaana baba mwenda pole.

Matibabu

Mwezi Novemba mwaka 2009 Bw Yar'Adua alikwenda kutibiwa Saudi Arabia. Alikaa hospitalini mjini Jeddah kwa kipindi cha miezi mitatu na hilo likazua mgogoro wa kikatiba nchini Nigeria. Katiba ya Nigeria inamhitaji makamu wa Rais kushika hatamu za uongozi wa nchi wakati Rais anapokuwa hawezi kutekeleza majukumu yake, lakini hilo linatakiwa kuandikwa rasmi na Rais mwenyewe, jambo ambalo Bw Yar'Adua hakulifanya. Raia wa Nigeria walielezea wasiwasi wao wakichagiza waelezwe hali ya Rais wao.

Akiwa kitandani hospitalini Bw Yar'Adua alikubali kufanya mahojiano na BBC. Hali hiyo ililifanya baraza la Senate la Nigeria kutumia sawa na tangazo kutoka kwa Rais wao kwamba hawezi tena kuongoza nchi na hapo wakafanya kikao cha kumwidhinisha makamu wa Rais Jonathan Goodluck kuchukua majukumu ya Rais, hata kama Rais hakukabidhi madaraka rasmi.

Ahadi za uchaguzi

Kati ya vigezo saba alivyovielezea kuwa mambo atakayoyatekeleza akiwa Rais, jambo moja lililoonekana kufaulu ni kuwashawishi makundi ya wapiganaji katika jimbo lenye mafuta la Niger Delta kuweka silaha chini na kujisalimisha. Kabla ya hapo kulikuwa na utekaji nyara mkubwa kwa raia wa kigeni wanaofanyakazi katika kampuni za mafuta.

Jambo moja ambalo lililowakera Wanigeria ni kwa yeye kushindwa kutekeleza ukomeshaji wa kukosekana umeme mara kwa mara.

Marehemu Yar'Adua alizaliwa mwaka 1951 katika familia iliyojikita katika siasa za Nigeria. Baba yake alikuwa waziri mara baada ya Nigeria kupata uhuru na kaka yake mkubwa alikuwa naibu wa Olusegun Obasanjo alipokuwa kiongozi wa kijeshi kati ya mwaka 1976 hadi 1979.

Yar'Adua alichaguliwa kuwa Gavana wa jimbo la Katsina, kaskazini mwa Nigeria mwaka 1999 na akachaguliwa tena mwaka 2003.