Maharamia waiteka meli ya Ugiriki

Maharamia wa Kisomali wameteka meli inayomilikiwa na Ugiriki katika ghuba ya Aden.

Meli Eleni P ilikuwa ikielekea Uchina, ilipovamiwa na maharamia.

Image caption Meli ya Eleni P

Mameneja wa meli hiyo, wanasema maharamia waliiteka meli hiyo iliyokuwa na mabaharia 23, wakiwemo Wafilipino 19 na Wagiriki wawili.

Eleni P, ilikuwa imesheheni chuma ghafi kutoka bahari nyeusi kuelekea Uchina. Hakuna ishara kuwa mabaharia walijeruhiwa wakati meli ilipotekwa.

Maharamia wa Kisomali wameteka meli kadha mwaka huu, ingawa kuna manuwari za jeshi la kimataifa kulinda eneo la Ghuba ya Aden.

Vita na serikali dhaifu nchini Somalia, zimesababaisha uharamia kuzidi katika mwambao wa nchi hiyo, na meli zimeshambuliwa mara kwa mara kwenye njia za safari baina ya Ulaya na Asia.

Siku ya Jumanne, baada ya kulipwa kikombozi, maharamia wa Kisomali waliiachilia huru meli ya mizigo, waliyoizuwia kwa miezi miwili.