Wanawake msiolewe na vijana au wazee

Wanaooana wakiwa na umri sawa huwa na maisha marefu

Utafiti mpya umeonyesha kwamba wanawake wanaotaka kuishi maisha marefu hawana budi kuolewa na wanaume walio na umri sawa.Kuolewa na mzee au kijana kuna fupisha maisha ya mwanamke.

Lakini habari njema kwa wanaume ni kwamba walio na wake wa umri wa chini wana nafasi ya kuishi maisha marefu na afya bora.

Ilidhaniwa wanawake ambao waume wao wana umri wa chini wanaweza kuishi maisha marefu.

Hata hivyo watafiti kutoka Ujerumani wamekanusha dhana hii baada ya kuwachunguza wenzi milioni mbili kutoka Denmark.

Kuolewa na mzee kunafupisha maisha ya mwanamke, na ni hatari zaidi kwa wanaoamua kuolewa na vijana walio na umri wa chini kuwashinda, kwani asili mia 20 yao hufariki.

Haijabainika sababu ya kuwepo kwa hali hii.

Baadhi wamesema wanawake walioolewa na wanaume wa umri wa chini kuwashinda wanakwenda kinyuma cha maadili ya jamii na mara nyingi hukumbwa na mafadhaiko.