Rais wa Nigeria apendekeza makamu wake

Namadi Sambo
Image caption Namadi Sambo aliyeteuliwa kuwa makamu wa rais Nigeria

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amemteuwa gavana wa jimbo la Kaduna Namadi Sambo kuwa makamu wa rais.

Bw Samba,mwenye umri wa miaka 57 sasa anasubiri kuidhinishwa na bunge la nchi hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kifo cha Rais Umaru Yar'Adua na kuapishwa kwa mrithi wake Goodluck Jonathan.

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema anayeteuliwa kuwa makamu wa rais anaonekana kuwa mgombea mwenye nafasi nzuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2011.

Bado haijabainika kama Bw Jonathan ndiye atapeperusha bendera ya chama tawala cha People's Democratic Party (PDP).

Bw Jonathan ni kutoka eneo la Kusini mwa nchi hiyo na chama cha PDP kimesema kitateuwa mgombea kutoka eneo la Kaskazini.

Bw Sambo ametokea eneo la Kaskazini lakini wachambuzi wanasema huenda Bw Jonathan akataka kubadilisha utamaduni wa chama hicho.

Uteuzi wa Bw Sambo umethibitishwa na msemaji wa jimbo la Kaduna Saidu Adamu ambaye amezungumza na BBC.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos Caroline Duffield anasema Bw Sambo hajulikani vizuri na hana ushawishi mkubwa wa kisiasa lakini anatarajiwa kuidhinishwa na bunge la Senate ambalo litakutana Alhamisi.