Kiongozi wa Madagascar hatagombea urais

Andry Rajoelina alitwaa madaraka kupitia mapinduzi

Kiongozi wa Madagascar Andry Rajoelina ametangaza kwamba hatagombea wadhifa wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba.

Kwenye taarifa iliyopeperushwa na runinga ya nchi hiyo, Bw. Rajoelina amesema amefikia uamuzi huo kwa manufaa ya taifa.

Kiongozi huyo alichukua madaraka kupitia mapinduzi hali iliyosababisha nchi hiyo kutumbukia katika msukosuko wa kisiasa.

Muungano wa Afrika ulitangaza vikwazo dhidi ya serikali ya Rajoelina na washirika wake.

Kiongozi huyo amekuwa akishinikizwa kutafuta suluhu dhidi ya mgogoro wa kisiasa ambao umekuwepo kisiwani Madagascar.

Bw. Rajoelina amekua akipinga pendekezo la kuundwa kwa serikali ya Muungano itakayowashirikisha mahasimu wake wa kisiasa. Hata hivyo wiki jana aliahidi kutangaza muelekeo mpya katika mazungumzo yaliyofanyika Afrika Kusini.

Kufuatia tangazo hilo serikali ya Ufaransa imempongeza kiongozi huyo kwa kuchukua hatua muhimu katika kusaidia taifa hilo kurejeea katika mfumo wa kidemokrasia.