Vitisho dhidi ya filamu ya Winnie

Utengenezaji wa filamu kuhusu maisha ya Winnie Madikizela-Mandela inayoigizwa na Jennifer Hudson inatarajiwa kuanza licha ya kuwepo vitisho vya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza katika tamasha la filamu la Cannes, mtengenezaji wa filamu hiyo Andre Pieterse amesema mawakili wa aliyekuwa mke wa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela alimwandikia barua.

Amesema barua hiyo ilikuwa na vitisho vinavyoweza kuzuia utengenezaji huo.

Filamu hiyo, iitwayo Winnie, pia inamhusisha Terrence Howard akiigiza kama Nelson Mandela.

Image caption Nelson na Winnie Mandela

Barua isiyo na madhara

Pieterse amesema barua hiyo pia imesema Bi Madikizela-Mandela "atapenda kuona mswada wa filamu na aidhinishe."

Lakini Pieterse amesema yeye na mkurugenzi Darrell Roodt waliamua filamu hiyo itazingatia utafiti yakinifu bila ya kuwa na ushawishi wowote kutoka wahusika wakuu.

" Ilikuwa barua dhaifu lakini pia ilikuwa na vitisho vya kushtakiwa, jambo linaloweza kuzuia filamu hiyo isitengenezwe."

Amesema: " Iwapo filamu hiyo itamkashifu kwa namna yeyote basi ataweza kuchukua hatua za kisehria."

Utengenezaji huo wa Winnie unatarajiwa kuanza tarehe 31 Mei nchini Afrika Kusini, itakayodumu kwa wiki 10.

Utekaji nyara

Bi Madikizela-Mandela alipata umaarufu wakati wa kipindi cha ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, alipokiongoza chama cha African National Congress ANC na kufanya kampeni ya kuachiwa huru kwa mumewe, aliyekaa gerezani miaka 27.

Image caption Jennifer Hudson na Terrence Howard

Ndoa yao ilivunjika miaka michache baada ya kuachiwa huru katika miaka ya 90.

Mwaka 1991, Bi Madikizela-Mandela alihukumiwa kifungo cha miaka sita kwa kuhusishwa na utekaji nyara. Baada ya kukata rufaa alitozwa faini badala ya kutumikia kifungo, lakini baadae alishtakiwa kwa makosa ya udanganyifu na wizi.

Roodt hakutaka kuzipa uzito taarifa hizo katika wasifu wa Madikizela-Mandela, na kuita uhusiano wa akina Mandela " Hadithi ya mapenzi ya kushangaza ya mwanamke anayejitolea kufanya lolote kwa ajili ya mume wake."

Hudson, aliyeshinda tuzo ya Oscar mwaka 2007 kwa kuigiza filamu ya Dreamgirls, amesema bado alikuwa anajifunza kuhusu Bi Madikizela-Mandela kabla ya kuigiza nafasi hiyo.

" Si jambo dogo kuigiza wasifu wa Winnie. Na ni jambo ninalolifurahia sana."