Wanawake wateseka na ubakaji Kongo

Wanawake wa Kongo
Image caption Wanawake wa Kongo

''Kiongozi wa waasi aliniuliza maswala mawili. Unataka tukuoe ama unataka tukubake?'"

Clementine aliyezaa watoto wanane anazungumza kwa upole na sauti ya kusitasita.

"Niliamua wanibake"

Anafahamisha : "Niliwaza moyoni mwangu ; nikiwaambia ningependelea kuwa mke wao basi wangemuua mume wangu. Sikutaka watoto wangu wakue huku wakisema kwamba mama yetu ndie aliyesababisha kifo cha mama yetu."

Lakini kujitolea kwake huko hakujasaidia kitu. Mume wake alimuacha na kumtafuta mwanamke mwengine.

"Baada ya kunibaka mume wangu alinichukia. Alisema nimekua mchafu.na kila mara hujiuliza: 'Sina shaka nilipoteza heshima yangu kwa ajili yake--sasa inakuaje ananitelekeza namna hii?

Margot Wallstrom, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ukatili katika mambo ya ngono amesema kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio" makao makuu ya ubakaji duniani".

Makundi mbali mbali ya wanamgambo yanazurura mashariki mwa Congo na yote yanatuhumiwa kwa kuhusika na ukatili dhidi ya wanawake.

'Kushindwa'

Clementine anasema hatukubali kuolewa kamwe: "Yeye ndie mume niliyemchagua katika ndoa tuliofunga kanisani. Mungu akipenda atarejea.''

Inaelekea kuwa ni ndoto ya kukata tamaa.

Jocelyn Kelly, mtafiti wa mpango wa kupambana na ukatili ,anasema wanaume ambao wameshuhudia ukatili huu dhidi ya familia zao nao pia wanaishi na kihoro:

"Wanasema:"Sitaweza tena kumuangalia mke wangu.' na kila mara wanapomuona mama huyu ,wanamuona mtu ambae hawakuweza kumlinda. Wanahisi kama wameshindwa kutekeleza jukumu lao kwa mama huyu na njia pekee ya kukabiliana na hali hii ni kumkataa mke wao na kuanza upya."

Haya ndio baadhi ya madhara yaliyosababishwa na watu kama Emmanuel, aliyekua askari utotoni na ambae sasa ni kijana wa umri wa miaka 22.

Image caption Waasi Kongo

Alikuwa mpiganaji wa kundi la waasi la CNDP.

Emmanuel anasema walibaka ili kuonyesha hasira zao dhidi ya serikali kwa kuwatelekeza.

"Wanajeshi au waasi kawaida hubaka kwa sababu tunakuwa mafichoni na hatupati mishahara yetu na hata tunapopata haifiki kwa wakati.

"Baada ya kuishi muda mrefu msituni huonani na wanawake, kwa hiyo mmoja akitokea basi sote hufaidika."

Silaha ya kivita

Lakini mwanaharakati anaetetea haki za wanawake nchini Congo Marie-Claire Faray anahoji kwamba wanaume kama Emmanuel wanatumilia hali duni ya wanawake. .

" Ikiwa hawawezi kujizuia basi wao ni sawasawa na wanyama "

Anasema, "Wanapigania kitu gani ? Hili haliwahusu wanawake,"

"Haiingii akilini. Wao wanapata starehe fulani na haihusiani na maslahi yoyote wanayoyatetea."

Ukatili wa ngono unatumiwa kama silaha ya vita. Ubakaji kwa magenge limekua jambo la kawaida na mara nyingine hutumia vitako vya bunduki.

Katika kituo kimoja mjini Goma Mashariki mwa Congo ambako manusura wa ubakaji wanaletwa kutoka vijiji mbali mbali ili kupewa huduma za matibabu,wanawake 57 wanaimba na kucheza ngoma.

Ngoma zao na vigelele vinaficha khofu yao.

Ingawa wamekwishakumbwa na maovu.

Kukosa hisia

Pembeni mwa chumba kimoja; harufu mbaya imehanikiza kama choo kisichosafishwa .

Harufu ilikuwa inatoka kwa akina mama wenyewe.

Baadhi yao wamekumbwa na maradhi ya fistula inayowafanya wasiweze kujizuia wanapokwenda haja iwe ndogo au hata kubwa.

Image caption Mwanamke Kongo

Msichana wa miaka 15-ameshughulika kupiga ngoma.

Na maisha yake ni kielelezo cha vita hivi visivyoeleweka dhidi ya wanawake.

Alitekwa nyara na waasi 10 wa kikundi cha Interahamwe ambacho kinashtumiwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari katika nchi jirani ya Rwanda. Na walimfunga kama mtumwa wao wa ngono kwa takriban mwaka mzima.

''Walikuwa wakinibaka kwa zamu na ilifika hadi sikuhisi tena maumivu.''

Walikuwa wakimlisha pale walipotaka wao na wakimpa maji ya kunywa kupitia mabuti ya mvua. Mara alipata mimba na waasi wanasema angeachiliwa huru mara baada ya kujifungua.

''Siku moja walinifunga kwa mti na kujaribu kumtoa mtoto...damu ilikuwa ikitiririka mtawalio.''

Anasema hawezi tena kusikia maumivu na anaelezea yote haya bila kuonyesha hisia za aina yoyote na kisha anajifunga shuka kiunoni na kuondoka.

Gerezani

Mwanajeshi wa zamani anaetumikia kifungo cha miaka 20 katika gereza kuu la Goma anasema alimshambulia mwanamke wa kwanza aliyekutana nae baada ya kutoroka kutoka kituo chake.

''Nilimuomba anisaidie. Nilikuwa na hii hamu ya kufanya ngono. Hakutaka kufanya ngono nami lakini nilimlazimisha. Nilihisi bila ya kufanya ngono basi ningekuwa mgonjwa.

"Aliondoka bila ya kulia lakini alipoondoka aliniambia kwamba angelinilaani.. Sasa najuta kwa sababu niko jela."

Ni miongoni mwa wachache ambao wamekamatwa.

Bi Kelly anasema wanajeshi wengi wanawachukulia wanawake kama ni wasaidizi wa wanaume.

"Kuna haya mawazo kwamba ni haki ya mwanamume kufanya ngono na haiwezekani mwanamume asifanye ngono."

Bi Faray anaelezea kuvunjika moyo: "Ikiwa hawawezi kujizuia basi wamefikia kiwango cha wanyama. Ni kisingizio tu cha kuhalalisha ukatili wao na wanaishi katika hali ya kutojali. Ni kisingizio cha kuishi maisha ya kihuni."

Dr Lucy Kasereka wa hospitali ya taasisi ya Heal Africa anasema ni vigumu kuipata haki. Hata hawa washukiwa wanapokamatwa hakuna gereza linalostahili au hata uwakilishi wa kisheria. Kwa sisi wakristo Amri Kumi ndizo zinazotuongoza''

'Waliangamiza maisha yangu'

Waziri wa sheria na haki za binadamu wa serikali ya kijimbo Francois Rucogoza anadhani ikiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itaweza kuvitokomeza vikundi vyote vya wapiganaji ndio ubakaji utamalizika.

Image caption Wanawake Kongo

Lakini wanawake kama Yvone, mwenye umri wa miaka 37, hataweza kusahau yaliyomfika.

Mume wake alilazimishwa kuangalia wakati akiwa anabakwa na kubakwa mtawalio. Hivi sasa mumewe hana haja naye.

Yvone anafahamisha :"Ninaishi na mume wangu nyumba moja lakini kila mmoja na kwake. Yeye ana kitanda chake nami nina kitanda changu pamoja na watoto.

"Hatuwezi kutenda tendo la ndoa. Ninapomwambia namtaka, yeye husema hapana haiwezekani.' Na kila tunapobishana huniambia nirudi kwa waume zangu Interahamwe.''

Anasema anamuomba mumewe aelewe hali yake. Lakini hakubali.

Ni wanawake wengine tu ndio wanamuelewa.

Clementine anazungumza kwa niaba yao wote anaposema.

"Sitawasamehe wabakaji hawa kwa sababu waliyaangamiza maisha yangu. Mara nyingine huhisi kama sina hamu ya kuendelea kuishi katika dunia hii."