Wanaume wapendanao wafungwa Malawi

Jaji mmoja nchini Malawi amewahukumu kifungo cha miaka 14 jela ikiambatana na kufanya kazi ngumu kwa wanaume wawili wanaofanya mapenzi ya jinsia moja kwa kosa la kufanya vitendo kinyume cha maumbile na vitendo vya aibu.

Jaji huyo amesema anataka "kuulinda" umma.

Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walikuwa gerezani tangu walipokamatwa Desemba 2009 baada ya kufanya sherehe ya uchumba.

Image caption Steven Monjeza na Tiwonge Chimbalanga

Kukamatwa kwao kulipingwa na nchi za kimataifa na kusababisha mjadala mkubwa juu ya mapenzi ya jinsia moja nchini Malawi.

'Wafungwa kwa imani zao'

Jaji Nyakawa Usiwa-Usiwa akiwa mjini Blantyre amesema, "Nitakupa hukumu itakayokutisha ili umma uweze kulindwa kutokana na watu kama nyie, ili tusije tukashawishiwa kuiga mfano huu wa kutisha."

Wakili wa utetezi Mauya Msuku ametaka watu hao wapunguziwe kifungo, akisema vitendo vyao havijamsumbua yeyote.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa siku ya Jumanne, " Tofauti na kesi ya ubakaji, kulikuwa hakuna aliyelalamika au aliyeathirika."

"Hapa ni watu wazima wawili waliokubaliana kufanya mambo yao kwa faragha. Hakuna atakayetishiwa wakiachiwa huru katika jamii."

Michelle Kagari, naibu mkurugenzi wa Afrika wa shirika la kimataifa la Amnesty, amesema hukumu hiyo "ni ya kikatili."

Amewaelezea watu hao kama "Wafungwa kwa imani zao" na Amnesty itaendelea kufanya kameni mpaka waachiliwe huru.

Malawi ni jamii yenye msimamo mkali ambapo mapenzi ya jinsia moja ni jambo la kuchukiza.

Jaji amesema mapenzi ya jinsia moja ni "Kinyume na maadili ya Mmalawi."

Lakini mtetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja wa Uingereza Peter Tatchell amesema sheria zilizotumika kuwahukumu watu hao ziliwekwa wakati Malawi ilipokuwa koloni la Mwingereza.

Amesema, " Sheria hizi zimetungwa na nchi za kigeni. Si sheria za kiafrika."

Watu hao walikana mashtaka na mawakili wao wamesema haki zao za kikatiba zimekiukwa.

Lakini kituo cha maendeleo ya watu (Cedep) na kituo cha haki za binadamu na kurekebisha tabia (CHRR) vimekuwa vikisihi mamlaka husika kulegeza msimamo juu ya wapenzi wa jinsia moja.

Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani wa Blantyre amesema serikali nayo inashinikizwa na wafadhili kutoka nchi za magharibi kuhusiana na suala hilo.

Anasema shinikizo hilo kwa nchi maskini kama Malawi ambapo bajeti yake inategemea asilimia 40 kutoka kwa wafadhili, si jambo dogo.