Bi Merkel abana usimamizi wa fedha

Bi Angela Merkel
Image caption Bi Angela Merkel

Kiongozi wa serikali ya Ujerumani, Chancellor Angela Merkel ametoa msisitizo wa kutaka hatua madhubuti za kudhibiti biashara ya fedha pamoja na benki.

Amesema serikali za mataifa makuu lazima zishirikiane na kutoa mfano wa umoja ili kudhibiti sheria kuhusu fedha.

Matamshi ya Bi.Merkel yanatolewa siku moja baada ya mataifa ya muungano wa Ulaya kukasirishwa na hatua ya Ujerumani kuchukua hatua ya kipekee kwa kupiga marufuku biashara ya muda mfupi katika masoko ya hisa.

Bi Merkel alionya pia juu ya hatari inayoikabili sarafu ya Euro endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa.

Kwenye kikao cha kimataifa mjini Berlin kinachofanyika kabla ya mkutano wa mwezi ujao wa G20 nchini Canada, Bi Merkel alitoa masharti kadhaa.

Moja ikiwa ni utaratibu makini wa kuongoza masoko ya kimataifa, akiongeza kuwa hili liwe msingi wa soko la bara la Ulaya pamoja na kodi kwa taasisi za fedha.

Serikali zilizomo kwenye muungano wa Ulaya zizingatie uangalifu katika matumizi yake ya fedha.

Mataifa yatakayokiuka utaratibu huu juu ya madeni na kukiuka takwimu za bajeti zao zichukuliwe hatua ikiwa ni kupunguziwa mchango kutoka muungano pamoja na kunyimwa haki yake ya kupiga kura.

Hata hivyo mwandishi wa BBC, Steve Rosenberg aliyopo mjini Berlin anasema wito huo unagongana na hatua ya Ujerumani kuchukua msimamo wa kipekee ili kuweka vikwazo juu ya biashara ya muda mfupi kwa masoko ya hisa.

Wakati huo huo waziri wa uchumi wa Ufaransa amesema haoni kama sarafu ya Euro inakabiliwa na hatari yoyote.