Mahakama za Kiislamu Kenya 'batili'

Jopo la majaji limeamua kwamba, kuwepo kwa mahakama za kiislamu nchini Kenya ni kinyume cha sheria na inaleta ubaguzi.

Image caption Waislamu wakiswali Mombasa

Majaji hao watatu wamesema mahakma hizo maarufu kama “mahakama za Kadhi” zimeipendelea Uislamu zaidi ya imani nyingine, na kwamba ilikuwa kinyume na katiba kwa kuwa Kenya ni nchi isiyotawaliwa katika misingi ya kidini.

Mahakama za kiislamu zimezua ubishani mzito katika katiba mpya iliyopendekezwa nchini humo.

Katiba hiyo inatarajiwa kupigiwa kura ya maoni mwezi Agosti mwaka huu.

Mahakama za Kadhi- zilizoanzishwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Mwingereza - aghlabu hushughulikia masuala ya ndoa na urithi kwa Waislamu wachache waishio Kenya.

Makanisa nchini Kenya yalifikisha malalamiko yao kuhusu suala hilo mahakamani miaka sita iliyopita.

Kama sehemu ya makubaliano ya kugawana madaraka ili kumaliza mgogoro kufuatia uchaguzi wa mwezi Desemba 2007, ilikubalika kuandikwa kwa katiba mpya.